- Wafichua taarifa waliozungumza na Mongabay wameripoti matukio ya ujangili yaliyodumu kwa miongo kadhaa, yanayohusishwa na kampuni ya uwindaji wa kifahari inayowahudumia watu wa tabaka la juu na familia za kifalme kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
- Watu wa ndani waliotoa taarifa hizi wana tajriba ya kazi kwa vitendo katika kampuni ya Ortello — inayojulikana pia kama Otterlo — Business Corporation (OBC), kampuni yenye makao yake UAE ambayo huendesha shughuli za uwindaji katika eneo la Loliondo, kaskazini mwa Tanzania.
- Mamlaka za Tanzania zimekuwa zikitangaza maagizo ya kuwaondoa wananchi mara kwa mara, hatua ambazo zimeathiri wafugaji wa Kimasai ndani na nje ya eneo la Loliondo, kama sehemu ya juhudi za kupanua uwindaji na utalii wa safari.
LOLIONDO, Tanzania — Kampuni ya uwindaji wa kifahari inayotoa huduma kwa watu wa tabaka la juu kutoka Falme za Kiarabu na familia ya kifalme, inadaiwa kuhusika na matukio ya ujangili yaliyodumu kwa miongo kadhaa hapa Tanzania, wafichua taarifa wameiambia Mongabay.
Wadau wa ndani wanatoka kampuni ya Ortello – wakati mwingine huandikwa Otterlo – Business Corporation (OBC), ambayo inaendesha shughuli zake huko Loliondo, wilaya ya Ngorongoro kaskazini mwa Tanzania.
Mahojiano na vyanzo vya habari, ambavyo viliomba majina bandia kwa sababu za kiusalama, yanatoa mwanga kuhusu safari za uwindaji zilizopangwa na kampuni ya OBC, ambazo zilivutia ndugu wa familia ya kifalme ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na washirika wao wa karibu angalau mara moja au mbili kwa mwaka kuanzia miaka ya 1990 hadi mwishoni mwa mwaka 2016. Wanaripoti kwamba baadhi ya safari hizi zilisababisha wanyamapori hai kusafirishwa kwenda nchi za nje kwa ndege.
Usafirishaji wa wanyamapori hai umepigwa marufuku nchini Tanzania tangu mwaka 2016 ili kulinda wanyama na ndege adimu. Mnamo mwaka 2022, wabunge walibatilisha haraka uamuzi wa kutatanisha wa kuondoa marufuku ambayo ilikuwa imewekwa kwa miaka sita.
Ushahidi wa vyanzo hivyo umekuja wakati mamlaka ya Tanzania imetoa notisi za kuwaondoa wafugaji wa Kimasai ndani na nje ya Loliondo, kama sehemu ya juhudi za kukodisha eneo la kilomita za mraba 1,500 (maili za mraba 580) kwa kampuni ya OBC.
Mwaka 2023, ripoti ya shirika la kutetea haki la Amnesty International ililaani vikosi vya serikali kwa vurugu na ukamataji wa watu wengi ambao uliwaacha wastani wa Wamasai 70,000 bila maeneo yao ya asili ya malisho.
Ili kuthibitisha madai ya wafichua taarifa kwa kiwango cha kuridhisha, tuliangalia eneo la uwindaji la kampuni ya OBC, tukafanya mahojiano na wakazi wa vijiji jirani na tukapata nyaraka za mahakama, hati za usajili wa kampuni pamoja na rekodi za usafirishaji.
Ikiwa na makao yake Dubai, kampuni ya OBC ilisajiliwa kama kampuni ya kigeni nchini Tanzania mwaka 1992 chini ya jina la biashara la Royal Safaris Conservation Co. LLC. Pia imesajiliwa katika mamlaka ya usiri ya Panama na Visiwa vya Virgin vya Uingereza.
Kampuni hiyo imewahi kushutumiwa kwa kutoa hongo nchini Tanzania, jambo lililosababisha kesi ya mahakamani ambayo baadaye iliisha kwa makubaliano ya maelewano. Pia imehusishwa na kufukuzwa kwa lazima kwa Wamaasai.
Kampuni ya OBC, wakurugenzi wake na mamlaka za Tanzania hawakujibu maswali yaliyoelekezwa kwao
Maficho ya wawindaji
Mongabay iliangalia eneo la uwindaji la kampuni ya OBC katika hifadhi ya wanyamapori ya Pololeti, Loliondo, na kuandika maeneo matatu ambayo wafichua taarifa waliripoti kuwa yalitumiwa na wageni mashuhuri wa Emirati.
Majengo hayo yanaonekana wazi katika nyanda kubwa za savanna ambapo swala, pundamilia na wanyama wengine asili huzurura.

Watalii wanaweza kumiminika katika mandhari hii kila mwaka ili kushuhudia makundi makubwa ya nyumbu wanaohama. Lakini kampuni ya OBC inahakikisha wanaopendelea kupiga risasi wanyama badala ya kutumia kamera kupiga picha, mahitaji yao yanatimizwa.
Miundo yake inaenea katika maeneo matatu: Chali One, eneo la juu la mlima linalotumika kama msingi mkuu wa watu maarufu wanaotembelea, lenye mnara wa mawasiliano ya simu na walinzi wa kudumu wa usalama; Lima One, kituo cha kuhifadhi na bohari ya magari; na uwanja wa ndege wa Lima Mbili na majengo.
‘Wageni’
Khalifa (jina bandia), alijiunga na kampuni ya OBC katika miaka ya 1990 na kufanya kazi huko kwa zaidi ya miaka 15. Mfanyakazi huyo wa zamani aliiambia Mongabay kwamba watalii hao wa Emireti walijulikana kama “wageni.”
Yeye na Abdulrazak (jina bandia), mfanyakazi wa sasa ambaye amekuwa OBC kwa zaidi ya muongo mmoja, waliripoti kuwa walishuhudia watalii wakivunja sheria za uwindaji katika safari zilizopangwa na kampuni hiyo, na kuua twiga na wanyama wengine wakionekana kutobagua wakati wa ziara zao Loliondo, ambazo zilipungua sana baada ya mwaka 2016.
“Kuna baadhi ya wanyama hawaruhusiwi kuwindwa, kwa mfano, twiga hawaruhusiwi kuwindwa kama sheria inavyosema, lakini wanawinda. Labda hawaogopi sheria za Tanzania. Wanajifanya kama watoto, wakiona mnyama akipita, wanachukua gari,” Abdulrazak alisema kuhusu wawindaji wa kitalii, akiiga sauti ya risasi. “Baada ya hapo, wanapiga picha.”

Alipoulizwa kwa nini hakuiarifu mamlaka ya Tanzania, Abdulrazak alisema hakuelewa kikamilifu kilichokuwa kikitokea mwanzoni.
“Ilionekana kama wamekuwa wakifanya hivi kwa miaka mingi, lakini hatukuelewa wanachofanya,” alisema.
Abdulrazak na Khalifa walidai kwamba walipotambua uzito wa kile kilichokuwa kikiendelea, walihofia kusema kutahatarisha maisha yao.
“Watu waliogopa,” Abdulrazak alisema. “Mbali na hayo, tungeripoti wapi?”
Abdulrazak alielezea Mongabay kwamba anaamini kuwa serikali ya Tanzania na polisi wamekuwa wakifahamu ukiukwaji wa uwindaji uliopangwa na kampuni ya OBC.
Mongabay iliiomba kampuni ya OBC na mamlaka za Tanzania kutoa maoni yao kuhusu madai hayo, na kueleza kama ruhusa yoyote maalum imetolewa kwa mauaji haya. Hawakujibu.
Kiukatili
Katika eneo la Chali One, eneo la kilima, Abdulrazak alisema alishuhudia jamaa wa familia ya kifalme ya Dubai akimpiga risasi twiga jike ambaye alitangatanga karibu sana na nyumba ya kuwinda.
“Niliona kwa macho yangu,” aliiambia Mongabay.
Twiga wa Kimasai (Twiga tippelskirchi), mnyama wa kitaifa wa Tanzania, ameoredheshwa kuwa katika hatari ya kutoweka na IUCN. Wahifadhi wanalaumu uwindaji haramu, magonjwa na uvamizi wa ardhi kuwa sababu za kupungua kwa idadi yake.
Adhabu ya kumuua twiga jike katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki inajumuisha faini ya hadi Dola 15,000 za Kimarekani, na kifungo cha miaka kadhaa gerezani.
Hata hivyo kulingana na Abdulrazak, hakuna hatua za utekelezaji zilizochukuliwa. Badala yake, alisema kuwa nyama kutoka kwa mnyama aliyekufa ilipelekwa Dubai.

Abdulrazak aliongeza kuwa alimwona mgeni huyo, ambaye alimtaja kuwa anajulikana sana miongoni mwa wafanyakazi wa kambi hiyo, mapema siku hiyo.
“Hakujitambulisha lakini tulimfahamu kwa jina lake,” alisema, akisisitiza kuwa anaweza kumtambua mtu huyo katika umati wa watu 500.
Mongabay ilimtaka mfanyakazi huyo wa kampuni ya OBC kumtambua mtu huyo kutokana na msururu wa picha zake, jambo ambalo alilifanya.
Abdulrazak aliendelea kusema kuwa matukio hayo ni ya kawaida miongoni mwa wawindaji wa hadhi ya juu (VIP), ambao, kama wenyeji, hutumia bunduki, mitego na mbwa kuwinda twiga kinyume na kanuni za wanyamapori zinazolinda wanyama hao.
Mizigo iliyofungiwa
Kampuni ya OBC ilianzishwa na Jenerali Mohammed Abdulrahim Al Ali, kutoka Emireti. Majaribio kwenye BRELA, jedwali la usajili la kampuni ya Tanzania, yanaonyesha anahudumu kama mkurugenzi wa kampuni ya Royal Safaris Conservation Co. LLC., jina la biashara la kampuni ya OBC, pamoja na mwananchi Khamis Mohamed Sultan bin Shaheen Al Suwaidi. Wanaume hao wawili hawakujibu maswali yaliyotaka kupata maoni yao.
Kwa mujibu wa Abdulrazak, Al Ali ndiye aliyekuwa mwanzilishi mkuu wa safari za uwindaji za watu wa hadhi ya juu wa UAE nchini Tanzania hadi 2016. Alikuwa na jukumu la kupanga ukamataji, kufungwa na kusafirishwa kwa wanyama hai, hasa watoto wa simba na chui. Haijulikani ni mara ngapi vitendo hivi vilifanyika au vinafanyika sasa.
Wakati huu, Al Ali alifanya kazi kwa karibu na Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, wadadisi wa kampuni ya OBC walisema. Waliongeza kusema kuwa Kinana alihudumu nafasi ya Kaimu Mwakilishi wa serikali ya Tanzania wakati wa ziara za watu wa hadhi ya juu Imirati.
Kulingana na watu kutoka ndani ya kampuni hiyo, Kinana na Al Ali waliratibu maandalizi ya ujio wa wageni hao, na kuwaagiza walinzi kubaini maeneo ya wanyama wanaowavutia. Wanaume wote wawili hawakujibu ombi la kutoa maoni yao.
“Abdulrahman Kinana yuko kila mara, hata Al Ali anapotembelea kabla ya wageni (kuwasili),” Abdulrazak alisema.
Mara nyingi, ulengaji wa shabaha uliishia kwa watalii kuua mnyama wa kike na kuwaweka watoto wake kwenye kituo cha kuhifadhia cha Lima One, kulingana na vyanzo.
“Wakikuona barabarani, wanakusimamisha na kukuuliza umeona wapi watoto wa chui, simba au mbuni,” Abdulrazak alisema kuhusu watalii hao. “Wanapenda sana wanyama wachanga kwa sababu wale wanyama wakubwa ni wagumu kusafirisha.”
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao, wakaazi wa Kirtalo na Ololosokwan, vijiji viwili karibu na hifadhi ya wanyamapori ya Pololeti, waliiambia Mongabay kuwa walishuhudia wafanyakazi wa kampuni ya OBC wakisafirisha wanyama hai kupitia ndege mwaka 2022 na 2023. Kando na hilo, Abdulrazak alisema kuwa kampuni ya OBC ilisafirisha wanyama hai kutoka Loliondo.
Kwa mujibu wa vyanzo viwili vya habari ndani ya kampuni ya OBC, wanyama wamekuwa wakisafirishwa kwa nyakati tofauti kutoka hifadhini hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ndege ndogo yenye uwezo wa kubeba vizimba kadhaa. Katika uwanja wa ndege, Al Ali na Kinana walisimamia uhamishaji wa wanyama hao kuingia kwenye ndege ya mizigo iliyokuwa inakwenda Dubai, walisema.
“Wageni wanapoondoka, ndege ya mizigo inaendelea kuchukua wanyama. Al Ali huondoka na safari ya mwisho baada ya ndege ya mizigo kuondoka,” Abdulrazak alisema.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ambayo ilichukua jukumu la kusimamia uwanja huo mnamo mwaka 2023, haikujibu ombi la Mongabay la kutoa maoni.

Kimbia au pigana
Kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2018 inatoa mwanga zaidi kuhusu oparesheni za kampuni ya OBC.
Kampuni hiyo iliingia kwenye mzozo na watu saba waliodai kulipwa na kampuni hiyo kusafirisha wanyamapori kupitia uwanja wa ndege. Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa kortini, ambazo hazijataja waziwazi shehena iliyobebwa, ajira yao katika kampuni ya OBC ilikatishwa isivyo haki mwaka 2016 na kudai fidia na malipo ya kuachishwa kazi. Kampuni ya Maendeleo ya Viwanja vya Ndege Kilimanjaro (KADCO), ambayo hadi hivi karibuni iliendesha KIA, ilikuwa imewapatia hati za usalama, nyaraka zinaonyesha.
Mahakama iliwapa malipo kamili ya suluhu, lakini uamuzi wa baadaye uliipendelea kampuni ya OBC baada ya kampuni hiyo kudai kuwa haikuwaajiri walalamishi. Kama ushahidi, ilitoa orodha ya wafanyikazi wake kipindi cha mwaka1998 hadi mwaka 2016.
Swali la nani aliyependekeza KADCO kuwapa hati za usalama – kampuni ya OBC au kampuni inayoshughulikia mizigo yake kwenye uwanja wa ndege – halijajibiwa.
Mahusiano ya karibu yanabakia
Ingawa ziara za kifalme zimeripotiwa kupungua tangu mwaka 2016, kampuni ya OBC bado ina uhusiano wa karibu na UAE.
Rekodi rasmi za mauzo ya nje ya Tanzania zilizopatikana kutoka katika hifadhidata ya biashara ya kimataifa zinaonyesha kuwa mwaka 2023, kampuni ya OBC ilisafirisha shehena 72 za nyama ya wanyamapori, au nyama ya porini, kutoka Tanzania hadi kwa angalau Waemirati wanne, wakiwemo viongozi wa biashara na washirika wanaofahamiana na UAE.
Tanzania ilihalalisha uuzaji wa nyama ya porini chini ya sheria kali mwaka 2020. Mongabay iliwasiliana na wapokeaji wa shehena hizo ikiwa na maswali kuhusu mauzo ya nyama hizo nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na iwapo vibali muhimu vipo.
Hakuna hata mmoja wa wapokeaji wanne aliyejibu swali lolote la Mongabay, na mmoja alitaja usiri kama sababu ya kukataa kutoa maoni. Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania pia haikujibu maswali ya Mongabay kuhusu uhalali wa mauzo ya nje. Wala kampuni ya OBC hawakufanya hivyo.
Historia sumbufu
Uwindaji wa watu maarufu wa UAE ulianza mwaka 1992, wakati serikali ya Tanzania ilipokodisha eneo la kilomita za mraba 4,000-km2 (1,544-mi2) huko Loliondo kwa raia wa UAE aliyetambuliwa kama Brig. Jenerali Mohammed Abdulrahim Al Ali.
Ardhi hiyo ambayo ina eneo la kilomita za mraba 1,500 ambayo mamlaka inataka kuikodisha, iliunda eneo lililokuwa likiitwa eneo la Pori Tengefu la Loliondo. Likawa eneo lenye matumizi mseto ya uwindaji, uhifadhi na ufugaji.
Masharti ya mpango huo yalikuwa siri ya serikali iliyolindwa kwa karibu. Lakini baadaye iliibuka katika ripoti ya tume ya serikali kuhusu ufisadi kwamba afisa aliyewaidhinisha alifanya hivyo kufuatia shinikizo kutoka kwa wakuu “kwa msingi kwamba yeye (Al Ali) alikuwa rafiki.”
Kufuatia kukosolewa na waandishi wa habari juu ya makubaliano ya kimyakimya, hasa kutoka kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Mfanyakazi Stanslaus Katabalo, ambaye makala zake muhimu juu ya mpango huo ziliibua kashfa iliyojulikana kama “Loliondogate,” Al Ali alianzisha kampuni ya OBC kama chombo cha kufanya mpango huo kuwa rasmi.
Kufikia 1994, Abubakar Mgumia, waziri wa utalii wakati huo, alipata shinikizo huku maelezo ya makubaliano hayo ya siri yakifichuliwa. Katika kukabiliana na hali hiyo, serikali ilianzisha Tume ya Marmo mwaka huo kuchunguza mpango huo huko Loliondo. Mgumia alifutwa kazi, lakini shughuli za kampuni ya OBC zilionekana kutoathiriwa.
Miaka miwili baadaye, Rais Benjamin William Mkapa aliunda Tume ya Warioba ili uchunguzi wa kina kuhusu ufisadi. Pia, iligundua kuwa leseni ya kampuni ya OBC haikuwa halali na iliunga mkono matokeo ya Tume ya Marmo kwamba hongo ilihusika katika ugawaji wake.
Leseni ya OBC ya kuwinda ilifutiliwa mbali mwishoni mwa mwaka 2017, huku kukiwa na madai zaidi ya hongo na ufisadi. Waziri wa Maliasili wakati huo, Hamis Kigwangalla, alimshutumu Isack Mollel, mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya OBC, kwa kujaribu kuhonga wizara yake na michango ya zaidi ya Dola za Kimarekani laki 2.
Mollel alikamatwa mara moja na kushtakiwa kwa uhujumu uchumi. Kulingana na nakala iliyochapishwa mnamo Aprili 2024, katika jarida la The Atlantic, kesi hiyo ilimalizika kwa makubaliano ya maombi.

Unyakuzi wa ardhi
Wanaobeba mzigo mkubwa wa uwindaji wa kitalii Loliondo ni wafugaji wa Kimasai, ambao wamekuwa wakifukuzwa mara kwa mara katika maeneo ya malisho ya asili tangu mwaka 1959, walipohamishiwa huko kutoka Hifadhi ya taifa ya Serengeti.
Wengi wa wale waliokimbia makazi yao sasa wanaishi katika maboma, makazi ya muda ya mapaa ya nyasi ambayo hutoa makazi kwa familia zao na mifugo, ambayo huvutia watalii wa kigeni kwa fursa za picha.
Mamlaka ya kikoloni iliwalazimisha Wamasai kuondoka katika makazi yao ya asili katika eneo ambalo sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kuweka maeneo hayo kwa ajili ya uwindaji wa kupangwa. Walikaa katika vijiji vilivyo pembezoni mwa mbuga.
Hifadhi zilibaki kuwa ndoto tu. Vikosi vya usalama viliwaondoa wanajamii katika vijiji vinne — Arash, Kirtalo, Oloirien na Ololosokwan — wakati wa oparesheni zilizofanyika mwaka 2009, 2013 na 2017, kulingana na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International.
Msako mkali uliendelea baada ya agizo la Rais mwaka 2022 kutangaza kuwa eneo la Pori Tengefu la Loliondo litakuwa hifadhi ya wanyama (Pololeti), na kusababisha vijiji 14 kuhama katika mchakato huo.
Mwaka huo, makabiliano makali yaliyotokea Ololosokwan, wilayani Ngorongoro, yalishuhudia polisi wakifyatua risasi kwa umati wa waandamanaji, na kuwajeruhi Wamasai kadhaa. Afisa wa polisi pia aliuawa kwa mshale.
Siku kadhaa baadaye, mamlaka za Tanzania zilitangaza kuwa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro itageuzwa kuwa pori la akiba, ambapo wafugaji hawaruhusiwi kuishi.
Kisha, Januari 2025, serikali ya Tanzania iliendeleza kampeni yake kali dhidi ya wafugaji wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi katika Bonde la Ufa. Askari waliwafyatulia risasi wafugaji wa Kimasai na kukamata ng’ombe wilayani Simanjiro karibu na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
Hapo awali, Mongabay iliripoti kwamba mnamo Machi 2024, mamlaka za Tanzania zilitoa notisi mpya za kuwafukuza Wamaasai kutoka katika maeneo yao. Awamu ya kwanza, kwa ajili ya kupanua Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, ililenga wilaya ya Simanjiro. Awamu ya pili iliathiri vijiji vinane kwa ajili ya kupanua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Picha ya bango: Twiga wakizurura katika hifadhi moja ya taifa nchini Tanzania. Ingawa wanyama hawa wanalindwa kisheria, ripoti zinaendelea kuibuka kuhusu jinsi wanakabiliwa na vitisho kutoka kwa wale wanaopuuza kanuni za uhifadhi. Picha kwa hisani ya Lars Jussaume, kupitia Flickr (CC BY-NC-ND 2.0)
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 22/08/2024.