- Wawindaji wa nyara nchini Tanzania waliwaua tembo dume wapatao watano waliokuwa na pembe zenye uzito wa zaidi ya pauni 100 (sawa na kilo 45). Tembo hawa maarufu, waishio katika Hifadhi ya Taifa ya Amboseli nchini Kenya,wanajulikana kwa tabia yao ya kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Tanzania, ambako uwindaji wa nyara unaruhusiwa.
- Wanaharakati wa uhifadhi walisema hadi mapema mwakajana kulikuwa na “makubaliano ya kiungwana” ambapo wawindaji walioko Tanzania hawakuruhusiwa kuwawinda tembo wa Amboseli hata walipovuka mpaka na kuingia Tanzania.
- Mradi wa Utafiti wa Tembo wa Amboseli, ambao umedumu takribani miaka 51, “ndio utafiti wa muda mrefu zaidi wa tembo duniani’’. Hii imewafanya tembo hao kuwa miongoni mwa tembo wanaofahamika zaidi duniani, wanafuatiliwa kwa karibu na wanafahamika zaidi na wanasayansi.
- Katika barua iliyochapishwa hivi karibuni kwenye jarida la Science, watu wapatao 24 waliotia saini walitoa wito wa kusitishwa kwa uwindaji wa tembo kutoka Hifadhi ya Amboseli wanaovuka kuingia Tanzania, wakisema kuwa tembo hao kutoka kundi hili “la kipekee” hawapaswi kuwindwa kwa ajili ya “kukidhi tamaa binafsi au maslahi ya kifedha ya muda mfupi.”
Wanaharakati wa uhifadhi wametoa wito wa kusitishwa kwa uwindaji wa nyara zinazotokana na tembo kutoka Hifadhi ya Taifa ya Amboseli nchini Kenya wanaovuka mpaka kuingia Tanzania, kufuatia kuuawa kwa zaidi ya tembo dume watano wenye mapembe makubwa isivyo kawaida na wawindaji nchini Tanzania.
Uwindaji wa nyara unaruhusiwa nchini Tanzania lakini ni kinyume cha sheria nchini Kenya. Chini ya kile wanaharakati wa uhifadhi walichoita “makubaliano ya kiungwana,” hadi sasa wawindaji hawatakiwi kuwagusa tembo wa Amboseli wanaozunguka mpakani mwa Kenya na Tanzania.
Utaratibu huo ulikuwa ni utambuzi wa umuhimu wa kundi hili la tembo wa savanna wa Afrika (Loxodonta africana), ambao wako katika hatari kubwa na idadi yao inaendelea kupungua. Mradi wa Utafiti wa Tembo wa Amboseli uliodumu kwa miaka 51 “ndio utafiti wa muda mrefu zaidi wa tembo duniani’’, jambo linalowafanya tembo wa Amboseli kuwa miongoni mwa tembo wanaojulikana zaidi duniani, waliopigwa picha mara nyingi na watalii, na wanaofahamika kwa undani na wanasayansi.
Kwa Cynthia Moss, anayeongoza Mradi wa Utafiti wa Tembo wa Amboseli, na Joyce Poole, mwanzilishi mwenza na mkurugenzi mwenza wa shirika lisilo la kiserikali la ElephantVoices, mauaji haya yaliwagusa moja kwa moja kwa kiasi kikubwa. Wote wawili walianza taaluma zao za kisayansi kwa kuchunguza kundi hili la tembo takriban miongo mitano iliyopita. Wanasayansi wamewapa majina karibu ya tembo wote 2,000 kutoka familia 69 wanaopatikana katika eneo hilo, wengi wao walizaliwa na kukua chini ya uangalizi wao wa karibu.

Matokeo ya mradi huu wa utafiti yameonyesha wazi tabia za tembo na maisha yao ya kijamii. Kadhalika matokeo ya utafiti ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa tembo huitana wao kwa wao kwa majina. Idadi ya tembo barani Afrika imepungua kwa kasi kubwa kutokana na ujangili, upotevu wa makazi yao ya asili, na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori. Hata hivyo, inaelezwa kuwa kuwaondoa madume makubwa kunaweza kuwa na athari kubwa isiyotarajiwa kwa kundi zima.
Makundi yenye maslahi kama vile mashirika ya uwindaji na yale ya uhifadhi mara nyingine huangalia zaidi mambo yanayoathiri idadi ya tembo kwa ujumla. Kutokana na hili, husahau umuhimu wa tembo mmoja mmoja katika jamii zao. Poole alisema kwamba madume wenye umri wa zaidi ya miaka 35 ni kama “nguzo kuu” katika jamii ya madume ya tembo. “Kama ilivyo kwa binadamu, huwezi tu kumtoa kiongozi katika jamii ukadhani kuwa haitakuwa na madhara,” alisema Poole.
Madume wa tembo waliokomaa husaidia kuelekeza tabia za tembo wa kiume walio wachanga, hasa wale walioko katika umri wa ujana. Uhai wa tembo hawa wa kiume — ambao wengi wao huendelea kuzaliana — ni muhimu sana katika kuhifadhi urithi wa vinasaba (genes) uliozalisha madume yenye sifa za kipekee. Tembo hawa hubeba vinasaba vya mapembe makubwa kupita yale yanayopatikana maeneo mengine.

Makubaliano yasiyo rasmi
Kwa mujibu wa wanaharakati wa uhifadhi, kuna sababu nyingine inayofanya kuwaondoa tembo hawa wenye mapembe ya kipekee kuwa wazo lisilo na tija. Tembo hawa huvutia kwa kiasi kikubwa watalii, na nchi kama Kenya na Tanzania ni maeneo muhimu ya utalii wa wanyamapori, na pia ni nyumbani kwa baadhi ya madume ya kipekee yanayoashiria urithi wa wanyamapori wa ukanda huu.
Biashara nyingi zinazoratibu safari za uwindaji pia hupanga matembezi ya kutazama wanyamapori. “Jambo la mwisho unalotaka ni mtu kumuua tembo anayehusishwa kwenye utafiti wa muda mrefu na kuharibu sifa ya tasnia nzima,” Poole aliambia Mongabay.
Kenya ilikuwa mojawapo ya nchi mashuhuri kwa uwindaji wa nyara kabla ya kupigwa marufuku mwaka 1977. Tanzania, ambayo ni jirani, inaendelea kuruhusu uwindaji wa nyara na hutoa vibali kwa waendeshaji wa safari kupitia mchakato wa zabuni. Kuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwindaji kandokando ya mpaka wa Kenya na Tanzania, na tembo wa Amboseli, ambao eneo lao la kuishi linazidi kilomita za mraba 30,000 (sawa na maili za mraba 11,600), sehemu kubwa ikiwa ndani ya Kenya, wanajulikana kwa kuvuka mpaka mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Moss, hadi hivi karibuni kulikuwa na “makubaliano ya kiungwana” ambapo wawindaji walioko Tanzania hawakutakiwa kuwalenga tembo wenye mapembe makubwa kutoka Amboseli. Makubaliano haya yalitokana na kutambua umuhimu wa tembo hao kama “viumbe wa utafiti,” na pia kwa sababu tayari wamezoea sana uwepo wa binadamu. “Kumpiga risasi tembo dume wa Amboseli ni sawa na kumpiga risasi mbwa wa kufugwa wa jirani yako,” Moss alisema katika taarifa rasmi.
Hata hivyo, kugunduliwa kwa mizoga ya tembo na wanaharakati wa uhifadhi nchini Tanzania, ambao waliwajulisha wenzao wa Kenya, kulionyesha mwisho wa makubaliano hayo ambayo hayakuwa yameandikwa popote. “Tulifanikiwa tu kumtambua tembo wa kwanza aliyeuawa,” alisema Moss. “Alikuwa tembo niliyemfahamu tangu alipozaliwa. Jina lake lilikuwa Gilgil.” Walifanikiwa kumtambua Gilgil kwa sababu mtu mmoja alipiga picha ya mzoga wake kabla haujachomwa moto. Moss alisema wawindaji walichoma mizoga hiyo ili kuzuia utambuzi.
Baada ya wawindaji kumuua wa kwanza kati ya tembo watano wanaojulikana kama “super tuskers”, jina linalotokana na mapembe yao kuwa na uzito wa zaidi ya pauni 100 (sawa na kilo 45), na kuyachukua mapembe yake ya kifahari, tukio hilo liliwavutia wateja wengine waliokuwa wakitafuta “nyara” zao binafsi.
Kwa kuwa hakuna makubaliano rasmi kati ya mamlaka za wanyamapori za nchi hizo mbili, utekelezaji wa suala hilo hutegemea tu kukubalika kwake na waendeshaji binafsi wa shughuli za uwindaji.
Mwaka 2023, kampuni mpya ilishinda zabuni ya uwindaji kwenye eneo la uwindaji lililoko karibu na Amboseli upande wa Tanzania. Tovuti ya Kilombero North Safaris iliweka tangazo lake ikiahidi “uzoefu bora wa safari za wanyama wakubwa nchini Tanzania.” Mtandaoni, makundi ya wapenda tembo wenye hasira wameacha maoni wakikosoa biashara hiyo na kutoa wito kwa wawindaji kuisusia. Kampuni hiyo haikujibu maombi ya maoni kutoka kwa Mongabay.

Wanyamapori walio kwenye utafiti
Mauaji ya tembo wenye mapembe makubwa wa Amboseli yanamulika mwenendo wa zaidi ya kampuni moja tu; yanadhihirisha ukomo wa jitihada za binadamu kutaka kuitawala dunia ya porini kwa kutumia sheria zilizotungwa na mwanadamu.
Tembo ni wanyama wanaozunguka maeneo makubwa. Tembo wa Amboseli huzunguka katika mandhari ya Amboseli hadi Magharibi mwa Mlima Kilimanjaro, eneo linalopakana na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro na kuvuka mpaka kati ya Kenya na Tanzania. Kwa makadirio, takriban asilimia 70 ya tembo barani Afrika huishi kwenye maeneo yanayovuka mipaka ya nchi mbalimbali. Kwa kuvuka mipaka hiyo ya bandia ya kibinadamu, tembo hujikuta katika mkanganyiko wa sheria za kimataifa za wanyamapori, ambazo huwachukulia wanyamapori kama raslimali za nchi wanamoonekana kwa wakati huo.
Hali hii huwa na changamoto zaidi pale ambapo mikakati ya uhifadhi ya nchi moja inakinzana na ya nchi nyingine, hasa katika masuala yenye utata kama uwindaji wa nyara.
Hili si suala la kisheria au kimahakama pekee kwa watetezi wa wanyamapori kama Poole. “Kwangu mimi inaonekana kuwa si sahihi hata kidogo kwamba wanyama wanaosafiri huru kuvuka mpaka wanapaswa kumilikiwa na mtu yeyote isipokuwa wao wenyewe,” alisema Poole. “Hawa ni wanyama wanaojitambua, wenye ufahamu, na wana uhuru wa kujiamulia, wana majina na huitana wao kwa wao.”
Katika barua iliyochapishwa kwenye jarida la Science, watu wapatao 24, wakiwemo Poole na Moss, walitoa wito wa kutaka zuio la muda la uwindaji wa tembo wa Amboseli nchini Tanzania. Ombi hilo halipingani na sera ya jumla ya Tanzania kuhusu uwindaji wa nyara. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya ndani, mwaka 2022 watalii waliokuja kwa ajili ya uwindaji wa wanyamapori nchini humo walichangia takriban dola za Marekani milioni 20 kupitia ada na shughuli nyingine zinazohusiana na utalii.
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) haikutaka kujibu maombi ya maoni ya Mongabay. Waungaji mkono wa sitisho hilo la muda waliwataja tembo wa eneo la Amboseli–Magharibi mwa Kilimanjaro kuwa ni “wa kipekee na wasio na mbadala,” wakisisitiza kwamba hawapaswi kuwindwa “ili kukidhi tamaa za kibinafsi au maslahi ya kifedha yenye faida ya muda mfupi.”
Picha ya Juu: Kutilia mkazo athari kwa idadi ya tembo mara nyingi hupuuza umuhimu wa kila mnyama mmoja mmoja katika jamii zinazoundwa na wanyama kama tembo. Picha kwa hisani ya ElephantVoices.
Nukuu:
Poole, J., Dobson, A., Bonham, R., Pope, F., Fishlock, V., Goodall, J., … Waruingi, L. (2024). Stop elephant hunting in Tanzania borderlands. Science. doi:10.1126/science.adq9074
Pardo, M. A., Fristrup, K., Lolchuragi, D. S., Poole, J. H., Granli, P., Moss, C., … Wittemyer, G. (2024). African elephants address one another with individually specific name-like calls. Nature Ecology & Evolution, 8(7), 1353-1364. doi:10.1038/s41559-024-02420-w
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 22/07/2024.