- Wahifadhi mazingira katika upande wa mashariki mwa Tanzania wamegundua aina mbili za miti adimu ambayo ilidhaniwa kuwa imetoweka.
- Miti aina ya Millettia sacleuxii ilitambulika katika aina sita katika misitu ya hifadhi ambayo karibu yote imetoweka.
- Kwasa sasa maelfu ya mbegu zimekusanywa na kupandwa na miche imeota na itapandwa katika Misitu ya Nguru kama sehemu ya mradi wa kufufua misitu hiyo.
- Miti miwili aina ya Milletti aliyohimili mabadiliko ya nyakati na ambayo imebaki kama wazazi imepatikana katika eneo ambalo wahifadhi wa mazingira wanatarajia kulifanya kuwa ushoroba wa wanyamapori.
Mwezi Julai 2023 mtaalamu wa mimea Andrea Bianchi alikuwa akiendesha gari katika Milima ya Nguru iliyoko mashariki mwa Tanzania ambapo aliona maganda makubwa ya matunda ya mti uliokuwa umeota katika shamba la mahindi lililokuwa kando ya barabara. Aliteremka na alipochunguza aliona miti miwili aina ya Millettia sacleuxii, aina ambayo wanasayansi walidhani imetoweka kabisa. Mpaka sasa maelfu ya mbegu yamekusanywa na kupandwa ili miche itumike kuboresha msitu na kuurejesha katika hali yake ya asili. Hii ini sehemu ya utekelezaji wa mradi unaolenga kuurudisha msitu katika hali yake ya awali.
Aina hii ya miti ni adimu kiasi kwamba haina jina katika lugha ya Kiingereza. Katika lugha ya Kihehe, mtu hutambulika kwa jina la ujumla tu na miti mingine ya jamii hiyo ya Millettia ambayo hupatikana katika eneo hilo. Wenyeji huitambua kwa jina la Muhafu.
Hapo awali wanasayansi walifahamu kuwa miti hii adimu ilikuwa ikipatika katika misitu ya hifadhi mitatu tu iliyopo katika milima ya Nguru na Usambara. Lakini misitu ya hifadhi miwili kati ya hiyo ilikatwa na kupotea miongo mingi iliyopita na badala yake kukawa na mashamba ya miwa na misitu ya miti ya kisasa ya mbao. Msitu mmoja wa hifadhi uliobaki ambao upo karibu na mji wa Turiani ni mdogo kiasi cha takriban hecta 49 (eka 121), nao unanyemelewa na wakulima wa mpunga na miwa.
“Nilipata wasiwasi mkubwa kuhusu aina hii ya miti, nikaogopa kuwa itakuwa imetoweka moja kwa moja,” alieleza Bianchi ambaye ni mtaalamu wa kurejesha uasili wa misitu ya kitropiki ambaye ndiye aligundua aina hiyo ya miti karibu na Mto Mvaji uliopo karibu na mji wa Turiani. Kwa bahati ya pekee, miti hiyo haikatwa kwaajili ya kujengea, kuni au kupisha kilimo kama ilivyokuwa kwa sehemu kubwa ya situ uliotoweka.
Moja kati ya miti hiyo ulikuwa umekingwa na mkuyu mkubwa na mwingine uliokuwa umbali wa karibu mita 50(futi 160) ulikuwa umezungukwa na nyasi na miti aina ya mitiki. Hii ina maana kuwa miti hii miwili haikuweza kustawi wala kufikia ukubwa uliotarajiwa. Lakini matunda yake yalitoa fursa mpya yakipekee ya kupanda miti mingine.
Mamia ya matunda yalipasuka na kusambaza maelfu ya mbegu wakati wa msimu wa kiangazi uliomalizika mwezi Oktoba. Mbegu elfu saba zilikusanywa na kuwekwa kwenye kitalu kilichosimamiwa na Bianchi na kikundi cha kuhifadhi mazingira cha PAMS Foundation. Kitalu hicho kilikuwa upande wa Kaskazini Magharibi mwa miteremko ya mlima Nguru. Eneo la Nguru ni mojawapo ya maeneo yapatayo kumi na mawili ambayo kwa pamoja yanaunda Safu ya Milima ya Tao la Mashariki. Kitalu cha miti kilichoanzishwa karibu na kijiji cha Pemba kimemsaidia mhifadhi kwa kushirikiana na baadhi ya wanakijiji kupanda mbegu ambazo kati yao 5,500 zimeota na kutoa miche yenye afya.


PAMS Foundation ndiyo inayoongoza utekelezaji wa mradi kwa kurejesha ubora wa baadhi ya sehemu za msitu wa Nguru ambazo zimeharibwa kutokana na ongezeko la shughuli za kilimo miaka ya karibuni. Mamia ya maelfu ya mbegu za aina mbalimbali 40 za miti ya asili zimepandwa.
Mradi huu unawashirikisha wakulima kutoka vijiji viwili ambavyo kwa makubaliano yaliyofikiwa wanaweza kukodisha sehemu ya mashamba yao kwa mradi ili zitumike kupanda miti. PAMS Foundation sasa wanaangalia uwezekano wa kujisajili na kuingia katika biashara ya hewaukaa kwa manufaa ya vijiji.
Miche ya Millettia ambayo ilipandwa mwezi Aprili “itakuwa sehemu maalum ya mradi wa kurejesha ubora wa asili wa mistu,” anasema Mkurugenzi Mwenza wa PAMS Foundation, Michele Menegon.
Miti aina ya Millittea sacleuxii ilitambuliwa na wanasayansi miaka 120 iliyopita na kupewa jina kwa heshima ya Mmisionari Mfaransa na mtaalamu wa mimea Charles Sacleux, lakini wakati huo ni miti michache tu ilitambuliwa. Kutoka na kutoweka kwa misitu ambamo miti hiyo ilikuwemo na kugundulika kwa miti miwili ambayo bado ipo nje ya msitu wowote wa hifadhi na kupanda maelfu ya miche yake, ina maana kuwa aina hii ya miti sasa imeokolewa na haitatoweka kamwe.
Mtu mwingine ambaye amewahi kutunza kumbukumbu ya miti hii katika karne hii ni mataalamu wa mimea Mtanzania aitwaye Moses Mwangoka. Alifanya hivyo mwaka 2004 huko Dunduma, sehemu ndogo iliyobakia ya uliokuwa msitu wa hifadhi karibu na Turiani ambao hata hivyo ulikuwa ukinyemelewa na wakulima wa mpunga na miwa.
Aliongea na Mongabay na kusema kuwa kuna uwezekano wa nusu kwa nusu wa miti ya aina hiyo kuwepo bado kwenye msitu huo. “Watu wamekuwa wakikata miti mingi. Nilipokwenda huko mara ya mwisho ilkuwa imebaki michache sana,” alisema. “Huenda kuna miti michache bado imesalia,” aliongeza na kutahadharisha kuwa Millettia ni miti migumu na inawavutia watu wanaotengeneza mbao.
Mwngoka alisema ana mpango wa kurudi tena Dunduma hivi karibuni kuona kama hiyo miti bado ipo.
Naye Bianchi ambaye hivi karibuni alikuwepo Dunduma kwa muda mfupi hakuona miti yoyote ya iana ya Millettia lakini alishuhudia msitu wa hifadhi ukishambuliwa na watu wanaotafuta kuni na watengeneza mbao.
“Msitu umekuwa kama tone la maji katika bahari ya mashamba,” alisema. “Ni matumaini yangu kuwa miti hii bado imo msituni ili tuweze kukusanya mbegu au hata chavua, iwapo mbegu hazitakuwepo.”
Chavua ni muhimu sana. Takriban asilimia moja ya miche ya Millettia ambayo Bianchi na wenzake walipanda kwenye vitalu kijiijini Pemba ilikosa rangi ya kijani ambayo inaifanya mimea kuvuta mwanga wa jua na kutengeza virutubisho ili iweze kukua.
Kukosekana kwa ukijani (chlorophyll), hali ambayo hujulikana pia kuwa uzeruzeru wa mimea, ni matokea ya kuzaliana kwa familia moja kunakotokana na kuwepo kwa jamii ndogo iliyotengwa.
“Tutaweza kuwa tumeokoa aina hii ya mti usitoweke,” alisema Biachi, “lakini tatizo la vinasaba bado litatupa wasiwasi.”
Kwa umuhimu wake, mahali ambapo Bianchi aligundua miti miwili ya Millettia ni karibu na mahali ambapo PAMS Foundation wanatarajia kurejesha ushoroba wa wanyamapori wenye upana wa nusu kilometa (maili0.3). Ushoroba huu utaunganisha Milima ya Nguru na Kanga, hifadhi inayolinda takriban hecta 7,000 (eka17,300) za msitu wa asili katika eneo tofauti liliko kati ya kilomita tano hadi kumi (kati ya maili tatu hadi sita) upande wa kaskazini mashariki.


Mongabay ilipotembelea eneo ambalo limepangwa kuwa ushoroba wa wanyamapori mwaka jana, iliona miti mirefu yenye magome meupe ijulikanayo kama sterculias (Sterculia appendiculata), au mfune kwa Kiswahili, ikionyesha kumbukumbu tosha ya hali ya miti ilivyokuwa hapo zamani.
Miti aina ya sterculias iliweza kumea hapa katika mashamba na msitu ulioharibiwa kwasababu aina hii ya miti haifai kwa mbao wala kuni.
Ushoroba huu utapita katika maeneo yemye maji na misitu na kuwavutia wanya makama (Atilax paludinosus) na (Aonyx capensis) ambao huishi karibu na mto, alisema Menegon.
Wahifadhi pia wanatarajia kuona wanyama kama Cephalophus spadix), na swala wadogo waishio misituni ambao wanapatikana Tanzania tu na hawajaonekana kwa miaka mingi.
Ushoroba huu pia unaweza kuwavutia tembo wanaoishi mbugani (Loxodonta africana) ambao kwa sasa wapo kaskazini na magharibi mwa Kanga baada ya kuhama kutoka maeneo ya Nguru.
“Kanga ina wanyama wengi wakubwa wakati Nguru ni mhanga wa ujangiri,” alisema Menegon. “Tunachotaka kujenga ni kwamba Kanga ndiyo iwe chanzo cha wanyama kurudi Nguru.”
Kufanikiwa kwa malengo haya kutachochewa na kurejesha kwa makazi ya wanyama kwa kutumia miche ya miti kutoka kwenye vitalu vilivyopo.
Menegon alitarajia kuwa pamoja na kurejeshwa kwa miti ya Millettia, aina nyingine ya miti huenda itakuwa ile ambayo bado hatujaigundua.
“Eneo la Nguru halijafahamika vizuri, hivyo huenda kwenye vitalu vyetu kukawa na miche ambayo wanasayansi hawajawahi kuitafiti. Hili ni jambo la kufurahisha sana”.
Picha ya bango: PAMS Foundation imeendelea kuandaa maelfu ya miche ambayo inapandwa katika ushoroba wa wanyamapori katika Milima ya Nguru iliyopo Tanzania. Picha na Andrea Bianchi.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kingereza mnamo tarehe 16/07/2024.