- Kukosekana kwa uhakika wa chakula kumeongezeka duniani kote kwasababu ya matukio hasi ya hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi na migongano.
- Ripoti ya hivi karibuni iliyochapishwa na IPES-Food inaonyesha kuwa masoko katika jamii mbalimbali ambayo ni sehemu ya utamaduni wa jamii za Kiafrika yanaweza kuongeza uhakika wa chakula na uwezo wa jamii kuhimili mabailiko ya tabianchi.
- Watafiti wameonyesha kuwa masoko yaliyoko katika jamii mbalimbali yanafikiwa kwa urahisi na watu wa kipato cha chini, na ambao pia huweza kumudu bei ya chakula katika masoko hayo. Masoko hayo pia hubadilika kulingana na hali halisi kuliko maduka makubwa ya vyakula, hasa linapokuja suala la upatikanaji wa vyakula mbalimbali vya asili, ambavyo huhimili mabadiliko ya tabianchi.
- Lakini kuna changamoto ya miundombinu, uwekezaji na usimamizi wa serikali, mambo ambayo kwa ujumla wake yanachangia kufifisha uwezo wa masoko hayo kutoa manufaa zaidi kwa watumiaji.
MBARE, Zimbabwe – Soko la mazao ya kilimo la Mbare lililoko nchini Zimbabwe, ambalo ni kubwa kuliko yote jijini humo, hufunguliwa saa 11 alfajiri na biashara kushika kasi mara moja. Kuanzia asubuhi hadi mchana, wafanya biashara kutoka sehemu mbalimbali ya nchi hufika sokoni hapo kuuza, pamoja na bidhaa nyingine, aina 100 za mboga na matunda ambazo huchambuliwa ili kusambazwa katika masoko mengine ya jijini na sehemu nyingine ya nchi.
Katika soko la Mbare bei ya bidhaa hupangwa asubuhi baada ya wauzaji kulinganisha kiasi cha na aina ya bidhaa zilinazopatikana siku hadi siku kulingana na msimu na mabadiliko ya tabianchi. Hapa ndipo asubuhi husikika kelele nyingi: wauzaji wakibishana au kujadiliana bei na wanunuzi ili kufikia muafaka. Bei ya bidhaa inaweza kubadilika kila siku.
Charles Dhewa, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa Knowledge Transfer Africa (KTA), shirika linalojishughulisha na maendeleo ya kilimo vijijini, hununua vyakula mbalimbali kutoka soko la Mbare.
Kitu kimoja cha kipekee katika masoko ya aina hii ni wingi na aina mbalimbali ya vyakula ambavyo vinapatikana, anaeleza Dhewa, ambapo maduka makubwa ya vyakula yaliyopo Harare, kwa mfano, huweza kuwa na labda tani kumi tu za viazi. Soko la Mbare huwa na zaidi ya tani 800.
“Jinsi vyakula vingi vya aina mbalimbali vinavyopatikana, ndiyo walaji hupata lishe bora na yakutosha. Kadhalika, kunapokuwa na vyakula vingi vya aina mbalimbali, bei hupungua na hivyo hata watu wa kipato cha chini huweza kupata mahitaji yao,” anaeleza Dhewa.
Wakati mashirikia ya kimataifa yakiendelea kutoa tahadhari juu ya ongezeko la wasiwasi wa uhakika wa chakula, ripoti iliyochapishwa tarehe 2 Julai mwaka huu inaonyesha kuwa uwekezaji katika masoko kama lile la Mbare ambayo yanawiana na mfumo wa kitamaduni wa Afrika ndiyo suluhisho la uhakika wa chakula. Masoko hayo huongeza utoshelevu wa chakula bila kuagiza chakula kutoka maeneo mengine. Pia huwahakikishia walaji uhakika wa chakula, huchochea kuhimili mabdiliko ya tabianchi na hivyo kuepusha ukosefu wa chakula na utapiamlo ambao huwakumba mamilioni ya watu duniani.
Zimbabwe, kwa mfano, inapambana na ukame mkali ambao haujawahi kutokea kwa miongo kadhaa, ambao umeathiri mazao ya nafaka nchini kote.Uvamizi wa Urusi huko Ukraine na athari zake kwa uzalishaji na uagizaji chakula kutoka nje ya nchi kumeongeza bei ya baadhi ya vyakula.
Dhewa anasema kwamba ili kukabiliana na hali hiyo wakulima nchini Zimbabwe wameanza kupanda nafaka za asili ambazo zinaweza kuhimili hali iliyopo, kama ulezi, ambao pia wanaweza kuuza katika masoko ya ndani.

Masoko ya ndani huwa karibu na nyumbani na mara nyingi huwa yako nje ya mnyororo wa masoko makubwa na wafanyabiashara wake ni wazalishaji wadogo, wasafirishaji na wachakataji wadogo. Masoko haya hutoa fursa kwa jamii kushiriki katika mfumo wake kama wazalishaji, wauzaji, wasafirishaji, wanunuzi na wachakataji. Lakini pia hutoa fursa kwa wakulima wa ngazi na vipato mbalimbali, wenye mfumo wa maisha tofauti na wenye umri tofauti. Wafanya biashara wanawake ndiyo wengi zaidi kwenye masoko haya.
“Kuwavuta wakulima wengi wa ngazi na vipato tofauti kunatoa fursa kwa washiriki kupata kipato na kuendelea kuzalisha vyakula vingine,” alisema Dhewa.
Kulingana na ripoti hiyo ambayo ilichapishwa na International Panel of Experts on Sustainable Food Sytems, IPES-Food, (Jopo la Wataalamu wa Kimataifa wa Mifumo Endelevu ya Chakula) lillilopo nchini Ubelgiji, mfumo wa chakula duniani umeshindwa kutatua vurugu iliyosababishwa na hali mbaya ya hewa isiyo kawaida, UVICO 19 na vita ya Ukraine.
Ingawa masoko ya ndani yanaathiriwa pia na mabadiliko ya tabianchi, uwezo wao wa hali ya juu wa kukabiliana na athari unawafanya waweze kusambaza vyakula kwa jamii kwa kukusanya vyakula kutoka sehemu nyingine za nchi ambazo hazikuathiriwa.
Maeneo yenye ukame nchini Kenya yamekuwa yakihimili vipindi vitatu vya ukame mkali katika muongo mmoja uliopita. Waathirika walitegemea chakula kilichopatikana kutoka katika masoko mengine ya nchi, kulingana na maelezo ya Edward Muiruri Kamiruj, Afisa programu wa PELUM Kenya. Huu ni mtandao wa vikundi vya wakulima wadogo.
Ukame mkali zaidi ulidumu kuanzia mwaka 2020 mpaka 2022, na kusababisha ugumu mkubwa wa maisha na watu kuhama kutoka sehemu wanazoishi ili kutafuta mahitaji ya masingi ya maisha.
“Maeneo mengi ya muinuko yaliweza kuzalisha kiasi kidogo cha mboga na viazi, mazao ambayo yaliweza kusafirishwa kwa malori kwenda kwenye masoko ya mijini na maeneo yenye ukame,” Kamirui aliiambia Mongabay. “Kwahiyo masoko ya ndani hayakuwa tu vyanzo vya kupata chakula bora lakini pia ndiyo msingi wa uhai wa watendaji wote katika mnyororo wa thamani wa shughuli mbalimbali.”
Watafiti wanasema kuwa masoko haya yanatoa fursa ya upatikanaji wa aina mbalimbali ya vyakula ambavyo huhimili mabadiliko ya tabianchi. Maduka makubwa siyo masoko ya vyakula vya asili, wamiliki hupenda kuuza vyakula vya kisasa vya kigeni, yakiwemo matunda na mboga za aina mbalimbali.
Vyakula vinavyouzwa ni vile vyenye viwango vya hali ya juu vilivyothibitishwa kwa alama au nembo fulani vikionyesha ukubwa, umbo na thamani yake ya jumla katika soko. “Hawana nafasi kwa ajili ya vyakula vya asili,” alisema Kamirui.
Lakini masoko ya ndani huuza kwa wingi matunda ya asili na bidhaa nyingine za kilimo ambazo ni za msimu na hazipatikani katika maduka makubwa.
“Masoko ya ndani huuza matunda ya ukubwa na ubora mbalimbali wakizingatia ukweli kwamba hakuna mkulima anayezalisha matunda ya ubora fulani au ukubwa fulani tu hata kama atakuwa makini sana au kutumia teknologia ya kisasa,” alieleza Dhewa.
Uwapi uwekezaji?
Mwezi May mwaka huu, nchi za Afrika Mashariki zilipata mvua kubwa kwa wiki kadhaa zilizosababisha mafuriko makubwa. Hali hiyo ilisababisha watu wengi kuhama makazi yao na jumla ya vifo 473.
Kenya, Tanzania, Ethiopia, Uganda na nchi nyingine zilikumbwa na maafa hayo mara mbili katika mwezi mmoja, hali iliyosababishwa na vimbunga vikubwa vilivyotokea katika Bahari ya Hindi na kuharibu miundo mbinu na mazao yaliyokuwa mashambani.
Licha ya uharibifu huo, baadhi ya wakulima waligundua kuwa mazao mengine ya asili kama mpunga, ulezi na bamia yalistawi vizuri sehemu zenye maji mengi. Waliyafungasha na kuyauza katika masoko ya ndani.
“Tuna zaidi ya aina sita ya matunda ya asili ambayo hayastawi endapo kutakuwa na mvua nyingi,” alieleza Dhewa. “Sasa wakati huu wa hali ya hewa ya El Niño kumekuwa na matunda mengi ya aina hii ambayo yanaweza kuuzwa kwenye masoko ya ndani tu.”

Kwa wakulima wadogo, biashara ya vyakula vya asili inakumbana na changamoto nyingi, ikiwemo kushuka na kupanda kwa bei kusikotabirika kwa sababu ya mabadiliko ya msimu wa uzalishaji, changamoto ya usafirishaji wa vyakula vinavyoweza kuharibika kwa haraka na ulanguzi katika biashara ambao huwakosesha wakulima faida, kulingana na utafiti uliofanywa. Katika baadhi ya masoko kuna biashara ya nyama pori ambayo wahifadhi wanapambana nayo kwa mafanikio haba.
Hata hivyo kulingana na ripoti ya IPES-Food, uwekezaji na usimamizi wa serikali katika masoko ya ndani ni mdogo. Duniani kote asilimia 70 ya mahitaji ya kifedha ya wazalishaji wadogo hayapatikani na kwa upande wa Afrika chini ya asilimia 10 ya wazalishaji wadogo hupata mikopo. Dhewa alieleza kuwa masoko yanakosa huduma muhimu kama maji salama na mifumo ya maji machafu. Hakuna majokofu ya kutosha ya kuhifadhi mboga na matunda ili yasiharibike.
“Hali hii inaathiri ubora wa baadhi ya matunda na mboga, kwani huharibika mapema. Changamoto nyingine ni usafirishaji. Vyakula vingi vya asili hupatikana katika maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi na hakuna usafiri wa kuaminika. Ni changamoto kubwa!” alieleza Dhewa.
Uwekezaji wa serikali kama ilivyo nchini Cameroon, umejikita katika uzalishaji mkubwa na siyo kwa wazalishaji wadogo ambapo mawaziri wanadai kwamba uzalishai mdogo haukidhi mahitaji ya chakula kwa ongezeko kubwa la idadi ya watu na hausaidii kukuza uchumi.
Kwahiyo wanaona bora kuwekeza kwenye mifumo na miundombinu ya uzalishaji mkubwa na biashara ya kimataifa ili kusimamia chakula kinachozalishwa. Lakini wataalamu wanadai kwamba kutowekeza kwa wazalishaji wadogo kunaathiri moja kwa moja masoko ya ndani ambayo huhimili mitikisiko ya uchumi wa dunia na mabdiliko ya tabianchi.
“Hili ni jambo ambalo liko wazi hasa kwa zama hizi ambazo mwenendo wa dunia hautabiriki. Hapa Afrika tunaishi kwa wasiwasi; hatuna uhakika wa jambo lolote, hivyo iko haja ya kuwa na mfumo ambao unaweza kuhimili au kuondoa kabisa mitikiso inayoikumba dunia,” alisema Million Belay, mratibu mkuu wa Alliance for Food Sovereignty Africa, shirika ambalo ni mwananchama wa IPES-Food, wakati akiongea na Mongabay.
Picha ya bango: Wenyeji wa Harare wakiwa katika Soko la Kilimo la Mbare kununua matunda na mboga zilizotoka moja kwa moja sahambani. Picha na Charles Dhewa.
Nukuu:
Balma, L., Heidland, T., Jävervall, S., Mahlkow, H., Mukasa, A. N. & Woldemichael, A. (2024). Long-run impacts of the conflict in Ukraine on grain imports and prices in Africa. African Development Review. doi: https://doi.org/10.1111/1467-8268.12745
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 27/04/2024.