- Wakulima nchini Kenya na nchi nyingine wanatumia vikundi vya gumzo mtandaoni na zana za akili mnemba (AI) kusaidia kukabiliana na upotevu wa mazao kutokana na wadudu na magonjwa.
- Utafiti mpya unaonyesha vikundi vya gumzo vilivyoundwa kwa mtindo unaofanana na vile vinavyotumika katika utunzaji wa afya ya binadamu vinaweza kuwa vya manufaa kwa wakulima na kuboresha mawasiliano yao na wataalam wa mimea.
- Mashirika kama vile PlantVillage na CABI yanatumia zana kama hizi za kidijitali na vikundi vya gumzo ili kupanua ufikiaji wao na kuongeza huduma zinazotolewa kupitia maafisa ugani na kliniki za mimea; wakulima wanaoshiriki wanasema ujuzi wanaopata kupitia zana za kidijitali unaweza kuwasaidia kuongeza mazao yao.
Huku mamilioni ya wakulima wakiteseka kila mwaka kwa sababu ya uharibifu mazao na vifo vya mifugo vinavyotokana na wadudu na magonjwa, baadhi ya wakulima barani Afrika wameanza kutumia teknolojia za hali ya juu, akili mnemba (AI) na zana za mtandaoni kama nyongeza ya huduma zinazotolewa na maafisa ugani katika kuwasaidia wakulima kukabiliana na hasara hizo.
PlantVillage (PV), shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu Marekani, ambalo linalenga kuboresha maisha ya wakulima na kuongeza tija ya kilimo duniani kote kupitia maarifa na teknolojia, ni mfano mmoja muhimu.
Programu ya shirika hilo inayoitwa AI PlantVillage hutumia teknolojia inayojulikana kwa jina la TensorFlow kutambua vitu kwenye majani ya mimea na mifumo inayoonyesha milipuko ya magonjwa. Chombo hiki ambacho kimetengenezwa kwa kutumia picha za majani ya mazao yenye afya na magonjwa, huweza kusaidia kutambua magonjwa na dalili za wadudu kwa mazao kama vile mahindi, mihogo, viazi mbatata, mtama na mengine mengi.
“Tuliunganisha mfumo wa akili mnemba (AI) katika programu zetu kwa sababu kutegemea maofisa ugani pekee katika eneo hilo kwa ufuatiliaji mara nyingi haitoshi,” Mkurugenzi Msaidizi wa PlantVillage Kenya, Lawrence Ombwayo, , aliiambia Mongabay katika mahojiano.
Alieleza kuwa programu hiyo ilitengenezwa ili kuboresha mfumo wa ugani wa shirika hilo, ikizingatiwa kuwa huduma za za ugani nchini Kenya na kote barani Afrika hazina raslimali. Shirika liligundua kuwa kutegemea tu maofisa wake wa ugani kulipunguza ufikiaji wake kwa wakulima, na hivyo kuzuia uwezo wa shirika la PV kusambaza taarifa kuhusu vitisho vya sasa na vinavyoibuka dhidi ya mazao pamoja na kupunguza ufuatiliaji wa changamoto zinazowakabili wakulima, Ombwayo aliongeza.

Kwa programu hii, wakulima wanaweza kutumia kamera za simu zao kushughulikia kwa haraka na kwa ufanisi masuala ya afya ya mazao. Kwa kuchanganua tu majani ya mazao kwa simu zao, programu inaweza kutambua magonjwa au matatizo papo hapo. Hii inawapa wakulima upatikanaji rahisi wa taarifa muhimu kuhusu afya na usimamizi wa mazao, na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi ambayo yanaweza kuongeza mavuno yao kwa kiasi kikubwa. Kwa sasa, programu imepata zaidi ya watumiaji 10,000 ambao waliripoti ongezeko la wastani wa asilimia 40 ya mazao, kulingana na PV.
Zaidi ya hayo, PV lina mfumo wa kutuma ujumbe mfupi yaani SMS na vikundi vya WhatsApp mtandaoni vilivyoenea katika kaunti 22 kati ya 47 nchini Kenya ambapo shirika hilo hufanya kazi. Kwa njia hii, wakulima wanapata kuwasiliana moja kwa moja kwa wakati na wataalam wa mimea, watafiti na maafisa ugani. “Kwa sasa, tuna vikundi vitatu vya WhatsApp hapa Machakos (kaunti) vyenye wastani wa wanachama 95 kwa kila kikundi,” alisema Cynthia Mukhwana, Mkuu wa Idara ya Entomolojia wa PV.
Wakulima wa PV nchini Kenya hawako peke yao katika kutumia zana kama hizi za kidijitali. Utafiti mpya unaonyesha kwamba watafiti wamepata ushahidi wa manufaa yanayoweza kutokea kwa kutumia vikundi vya gumzo mtandaoni miongoni mwa wakulima na madaktari wa mimea kushughulikia masuala ya kawaida ambayo wakulima hukabiliana nayo.
Utafiti huo, uliochapishwa Machi katika jarida la CABI One Health, unachambua fursa na vikwazo vya kutumia vikundi vya gumzo mtandaoni kwa mifumo ya afya ya mimea sawa na vikundi vya gumzo ambavyo hutumiwa sana katika utunzaji wa afya ya binadamu. Kwa mfano, mazungumzo ya kikundi yamewezesha wagonjwa kupata mara moja watoa huduma za afya. Ikiwa kuna matatizo yoyote, kuweza kuzungumza na mtaalamu au wanajamii wengine kunaweza kusaidia sana wagonjwa.

Baadhi ya wakulima na madaktari wa mimea wanafuata mfano huo, kwa kutumia vikundi vya gumzo mtandaoni ili kuimarisha mawasiliano.
“Tuna mpango unaoitwa PlantwisePlus ambapo tulianzisha kliniki za mimea katika mataifa mengi duniani ili kutoa huduma za ushauri kwa wakulima,” alieleza Dannie Romney, mmoja wa waandishi wenza wa utafiti huo aishiye nchini Kenya, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kimataifa wa Mawasiliano ya Maendeleo na Ugani katika shirika la CABI, shirika lisilo la kiserikali la kimataifa ambalo linatumia sayansi kutatua matatizo katika kilimo na mazingira.
Aina hizi za kliniki za mimea ni “njia mpya ya kusaidia usimamizi wa afya ya mimea,” inayotegemea “madaktari waliopatiwa mafunzo maalum ya kuchunguza na kutoa matokeo ya kisayansi kuhusu namna ya kudhibiti wadudu na magonjwa ya mimea kulingana na ushahidi kutoka kwa sampuli za mimea iliyoathiriwa, inayoletwa na wakulima kwenye kliniki hizo kupanda,” waandishi wa utafiti wanaandika. Programu za kidijitali zinatumika kuongeza wigo wa huduma hizi.
“Tumefanya kazi kwa karibu sana na ofisi za ugani za serikali katika nchi na kuzisaidia kuendesha kliniki za mimea, ambazo zimebuniwa kwa mfumo wa huduma za afya ya binadamu, ambapo kulikuwa na kliniki zilizoko tayari kutoa huduma, na wakulima wenye tatizo, walikuwa na fursa ya kufika na kushauriana na mtaalamu,” Romney alisema.
Hapo awali, alisema, shirika la CABI lilitumia mfumo wa karatasi kwa ufikiaji wake. Lakini baada ya muda, shirika lilianzisha zana za kidijitali kusaidia ukusanyaji wa data, lilitoa kompyuta za mkononi na kuanza kutumia Telegram, programu inayofanana na WhatsApp, ili kurahisisha mawasiliano na wakulima.
Hata hivyo, ufanisi wa vikundi vya gumzo vinavyotumika miongoni mwa jamii za wakulima haukuwa umechunguzwa kwa kina, kwa hiyo watafiti waliazimia kufanya hivyo kupitia mapitio ya maandiko, uchunguzi wa vikundi vya gumzo mtandaoni na tafiti kwa njia ya dodoso kwa washiriki walioko nchini Kenya, Ghana, Uganda na Sri Lanka.

Utafiti wa awali uliweka wazi manufaa ya vikundi vya gumzo vya huduma ya afya ya binadamu mtandaoni, ikiwa ni pamoja na “kuwezesha mawasiliano bora kati ya wataalamu wa afya, kuunganisha idara tofauti ndani ya hospitali, hospitali na hospitali zingine, na wataalamu wa vijijini na wataalamu wa mijini,” waandishi wa utafiti huo wanaandika. “Matokeo yetu yanaonyesha kuwa kuna ushahidi unaothibitisha kuwepo kwa manufaa ya vikundi vya gumzo kwa afya ya binadamu ambayo inaweza kuigwa katika afya ya mimea,” Romney alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Vikundi vya gumzo vya telegram “viliongeza ufanisi wetu kwa kiasi kikubwa, hasa kwa kliniki za mimea,” Romney aliiambia Mongabay. “Kliniki hizi sio tu ziliwafikia watu moja kwa moja kwenye tovuti lakini pia zilisaidia vikundi vya gumzo kuunda mtandao wa wafanyakazi wenzao na wataalam. Mtandao huu uliruhusu mashauriano na kuboresha huduma, kupanua ufikiaji wetu na matokeo chanya.”
Mwaka 2021, shirika la CABI lilichapisha sura katika kitabu kilichoitwa The Politics of Knowledge in Inclusive Development & Innovation, ambayo ilifichua kuwa, “Kwa kujitolea kwao wenyewe, madaktari wa mimea walianza kutumia makundi haya ya mawasiliano kwa njia ya mtandao kuwasiliana kuhusu mada mbalimbali, wakishiriki uchunguzi juu ya matukio ya wadudu waharibifu wa mimea, kutafuta ushauri wa namna ya kutibu wadudu wasiotambulika, kujadili masuala ya kiutawala, na pia kujumuika kijamii na wenzao.”
Maeneo haya ya mtandaoni “yaligeuka kuwa vikundi vya kitaifa vya msaada baina ya wakulima na madaktari wa mimea waliotawanyika kijiografia, huku pia yakipokea mchango kutoka kwa wataalamu wa kitaifa katika ulinzi wa mimea na utafiti.”
Kwa maneno ya Romney, makundi ya mazungumzo ya mtandaoni kwenye Telegramu yanatumika kama “mfumo wa tahadhari ya mapema,” ambapo wakulima hujadili matatizo wanayokumbana nayo shambani. Kupitia makundi haya, washiriki wamekuwa wakituma picha za mimea yao iliyoathirika huku madaktari wa mimea wakibaini matatizo hayo na kutoa mapendekezo ya matibabu dhidi ya magonjwa ya mimea. Hii imesababisha ongezeko la mavuno kwa wakulima ambao ni sehemu ya mpango huu.
“Mwaka 2018 hadi mwaka 2019, tulipokuwa tukifanya kazi kwa ajili ya chapisho hili , tulifanya tathmini ya athari za kliniki nchini Kenya na ufanisi wake,” Romney alisema. “Cha kufurahisha, katika kipindi cha utafiti, kulitokea mlipuko wa viwavijeshi (FAW). Tulichogundua ni kwamba katika maeneo ambayo kulikuwa na zahanati na maofisa ugani waliopewa mafunzo ya udaktari wa mimea, wakulima walipata ongezeko la asilimia 13 la mavuno na kipato ikilinganishwa na maeneo yasiyo na huduma hizo. Hii inadhihirisha faida kubwa ya kliniki za mimea katika kuongeza tija ya kilimo na maisha ya wakulima,” alisema.

“Watu mara nyingi huhusisha mitandao ya WhatsApp na Telegram na mazungumzo ya kawaida tu,” Romney alisema. “Hata hivyo, utafiti wetu uliangazia jinsi majukwaa haya yanavyoweza kuleta pamoja vikundi vya watu kwa ufanisi ili kuboresha kazi zao” na kushughulikia masuala mazito.
Hili ni kweli kwa shirika la PV, ambalo pia hutumia makundi yake ya mazungumzo kuelimisha wakulima kuhusu kazi yake ya udhibiti wa wadudu kwa njia jumuishi. IPM, kama inavyojulikana, inalenga kupunguza uharibifu wa wadudu kwa njia ya gharama nafuu zaidi huku ikipunguza hatari kwa watu, mali na mazingira. Kupitia makundi ya mazungumzo, PV huwafahamisha wakulima kuhusu mipango yake ya IPM, ikiwapa taarifa za kisasa kuhusu mzunguko wa maisha ya wadudu na jinsi wanavyoingiliana na mazingira. PV pia hutumia majukwaa ya mtandaoni kuwasiliana na wakulima wanaotumia bidhaa za shirika hilo, kama vile mbolea ya biochar. (Hata hivyo, kwa kuwa si wakulima wote wana simu janja, kundi hili bado huendesha warsha za ana kwa ana pia.)
PV lina maabara kuu tatu na maabara ndogo mbili kwa ajili ya programu za utafiti za IPM. Moja ya maabara hizi iko Tala, katika kaunti ya Machakos, eneo la mashariki mwa Kenya, takriban kilomita 56 (maili 35) mashariki mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Hapa, idara ya sayansi ya wadudu inajikita katika uzalishaji mkubwa wa vimelea ili kukabiliana na viwavijeshi yaani FAW, ambavyo ni tishio kubwa kwa wakulima wa mahindi (Zea mays), chakula kikuu nchini Kenya. Kimelea ni kiumbe anayeishi kwa uhusiano wa karibu na mwenyeji wake, na hatimaye kusababisha kifo cha mwenyeji. Shirika la PV lilitambua maadui wawili wa asili wa viwavijeshi yaani FAW: Trichogramma chilonis na Telenomus remus.
Sampuli za vimelea hivi vya asili zilikusanywa na kuletwa kwenye maabara ya PV kwa ajili ya kuzaliana kwa kiasi kikubwa. Ili kuwezesha mchakato huu, idara ilichagua aina mbili zinazofaa: viwavijeshi yaani FAW na nondo ya mchele, ambayo watafiti hufuga kwa ajili ya mayai yake na baadaye hupitiwa na vimelea ili kuzalisha vimelea zaidi.
Mayai yanaenezwa sawasawa kwenye kadi za pembe kwa kutumia gundi isiyo na harufu. Baada ya kutayarishwa, kadi hizi huwekwa wazi kwa vimelea. “Ili ugonjwa wa vimelea kutokea, vimelea hutaga mayai yake ndani ya mayai ya viwavi jeshi. Watoto wa vimelea hula vilivyomo ndani ya mayai ya viwavi jeshi, na kukamilisha ukuaji wao ndani ya siku kuanzia 7 hadi 10, kulingana na hali ya joto, kabla ya kuibuka kama vimelea waliokomaa,” Mukhwana alibainisha.
Ili kuwapa wakulima vimelea kwa ajili ya matumizi kwenye mashamba yao, kadi zilizoandaliwa huwekwa kwenye bahasha na kusafirishwa hadi kwenye mashamba siku moja kabla ya vimelea hao kutoka kikamilifu. Mara baada ya kuachiliwa, vimelea vinaungana na kundi la viumbe wa eneo hilo, hupata mayai ya viwavi jeshi na kuyawekea vimelea. Kila kadi inauzwa kwa shilingi 300 (takriban dola za Marekani 2.30).
“Hapo awali tuligeukia vimelea vya shirika la PlantVillage wakati wa mlipuko mkali wa viwavi jeshi,” mkulima Diana Kimani aliambia Mongabay. “Wakati huo, tulitegemea dawa za kuulia wadudu kwa shamba letu la mahindi la ekari 3, ambalo lilionekana kuwa ghali sana.” Alifafanua kwamba dawa waliyokuwa wametumia iliuzwa katika chupa za mililita 100 (3.4-fluid-ounce) kila moja ikigharimu shilingi 700 (dola za Marekani 5.42), na ilihitaji kuizimua kujaza ndoo 10. Suluhisho hili lilihitaji kunyunyiziwa angalau mara sita kabla ya kuvuna, bila kujumuisha nguvu kazi na gharama za ziada.


Kinyume chake, kutumia vimelea kulihitaji kadi 12 tu ili kuondokana na uvamizi, na kupunguza kwa kiasi kikubwa haja ya kunyunyiza mara kwa mara. Mbinu hii ilileta mavuno bora ya mahindi ikilinganishwa na msimu uliopita.
Mbali na mikakati ya IPM, idara ya maikolojia ya PV, ambayo inafanya utafiti wa kina katika matumizi ya fangasi wenye manufaa kuua mabuu ya viwavi jeshi yaani FAW, pia huuza mbolea ya biochar kwa shilingi 1,800 (dola za Marekani 13.95) kwa gunia la kilo 50 (pauni 110). “Tulitaka kuwapa wakulima njia mbadala ya uhakika, kwa hiyo ni mpango kamili,” alisema Mercy Kemboi, kiongozi wa idara hiyo.
Mkulima Jemimah Kioko, anayetumia mbolea ya biochar, alizungumzia manufaa ya shamba lake la ekari 7, ambapo yeye hupanda kahawa, mahindi na mazao mengine mbalimbali. “Mwanzoni mwa mwaka huu, nilisafiri nje ya nchi kumtembelea binti yangu na nilichelewa kuanza kupanda. Shirika la PlantVillage lilinipa mbolea ya mimea, ambayo niliiweka kwenye shamba langu la mahindi. Sasa, mazao yanastawi,” alisema.
Kazi hizi zote ni za kukupa mawazo makini katika mijadala ya kikundi cha mazungumzo ya wakulima kama ilivyobainishwa na wakulima waliotajwa hapo juu. Walifichua kuwa vikundi vya WhatsApp ambavyo walikuwa sehemu yake viliwasaidia kupata taarifa mpya. Na vikundi hivi pia vilitoa jukwaa la kuuliza maswali ya ufuatiliaji kuhusu bidhaa za PV walizotumia kwenye mashamba yao.
Jambo moja ambalo wataalamu wa PV wameona ni kwamba ushiriki wa kikundi cha gumzo huathiriwa na mambo kama vile misimu ya kupanda. Kwa mfano, wakati wa misimu ya upandaji wa mahindi au maharage (Miezi ya Machi-Mei wakati wa mvua ndefu au Miezi ya Oktoba-Novemba wakati wa mvua fupi), wakulima huchangamka sana, wakiuliza maswali kuhusu magonjwa yanayoathiri mazao yao. Lakini katika msimu wa mbali (Miezi ya Desemba-Februari), ushiriki wao huwa mdogo sana.
Ili kukabiliana na hili, PV huandaa mafunzo mbalimbali kwa wakulima. “Wakati wa msimu wa baridi, mafunzo mengi hufanywa na wakulima ili kuweka mtiririko wa taarifa, kwani wakulima wakati huu wanaandaa mashamba yao kwa msimu ujao wa kupanda.”
Kushiriki video fupi za kilimo au elimu ya masuala ya ugani katika vikundi pia husaidia kudumisha mazungumzo, kwa kuwa mara nyingi wakulima huuliza maswali kuhusu video fupi za kilimo.
Ingawa linakubali ukosefu wa upatikanaji wa simu mahiri kwa baadhi ya wakulima, wakati mwingine PV huwafundisha washiriki kuwa “wakulima wakuu” ambao baadaye watawaelimisha wenzao juu ya kile walichojifunza. Baadhi ya wakulima hawa ambao ni wazuri sana katika kushiriki habari huishia kuwa mawakala wa shirika. Kwa sasa kuna mawakala 11 huko Machakos, huku Diana Kimani akiwa mmoja wao. “Kama wakala, ninazunguka kuwaelimisha wakulima kuhusu bidhaa zetu, matumizi yake na faida zake,” alisema.
Kimani alipokea simu janja kutoka PV, ambayo anaitumia kurahisisha mawasiliano na wakulima aliowafundisha na kufuatilia mauzo ya bidhaa alizopangiwa. Kila wakala anawajibika kuuza idadi maalum ya bidhaa, kama vile mifuko 10 ya mbolea ya mimea, ndani ya muda uliowekwa. Hata hivyo, Kiani bado anaendesha baadhi ya vipindi vya mafunzo vya ana kwa ana kwa sababu si wakulima wote wanaoweza kupata simu au simu janja. Ukosefu huu wa ufikiaji unasalia kuwa kikwazo kikubwa cha kutumia kikamilifu zana za kidijitali na vikundi vya gumzo kwa ajili ya kuboresha afya ya mimea.
Picha ya bango: Mkulima Florence Ochieng akivuna mahindi mabichi huko Trans-Nzoia, Kenya. Picha na CIMMYT, Peter Lowe kupitia Flickr (CC BY-NC 2.0)
Nukuu:
Jomantas, S., Wood, A., Munthali, N., Ochilo, W., Thakur, M., Romney, D., & Kadzamira, M. (2024). Looking at human healthcare to improve agricultural service delivery: The case of online chatgroups. CABI One Health. doi:10.1079/cabionehealth.2024.0008
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 27/06/2024.