- Mabwawa ya mafunjo yaliyo katika kingo za Ziwa Viktoria, Afrika Mashariki, yamekuwa chanzo cha riziki kwa vizazi vingi vya jamii zinazoishi humo.
- Baadhi yao huvuna mafunjo hayo kutengeneza mikeka, vikapu na bidhaa za mikono, huku wengine wakitegemea uvuvi wa samaki wanaozaliana kwenye maeneo yaliyo ndani ya mafunjo hayo.
- Mabwawa hayo pia ni makazi ya ndege wanaoishi katikati ya mafunjo katika eneo dogo kijiografia, huku vichaka hivyo vya miwavi vikifanya kazi ya kuchuja virutubisho na kushikilia mashapo — hali ambayo pia inachangia uhifadhi wa kaboni kila kunapoongezeka mabaki ya mimea na mashapo ya ardhi oevu.
- Hata hivyo, shinikizo la maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa hoteli mpya na upanuzi wa mashamba limehatarisha mfumo huu wa ikolojia, huku kuingizwa kwa samaki aina ya sangara (Nile perch) kwenye ziwa hilo miaka ya 1950 kukitokomeza vizazi vya spishi nyingi asilia.
Kadri jua linapochomoza kwenye maeneo oevu ya Ziwa Viktoria, wavunaji wa mafunjo wanaonekana wakiingia kwenye mabwawa kuyavuna. Ufukweni, wavuvi ambao wamemaliza shughuli za usiku pia wanavuta mashua zao. Sauti tamu za ndege aina ya papyrus gonolek (Laniarius mufumbiri) pamoja na milio ya ndege wakubwa jamii ya coucal (Centropus monachus) zinasikika vikitoka kwenye mifunjo.

Sauti za ndege, binadamu, samaki pamoja na miti ya mafunjo iliyopangwa juu vyote vinaashiria mfumo wa ikolojia unaostawi. Mabwawa haya ya kingo za Ziwa Viktoria na mito mingine ya eneo hili, ni hifadhi ya ndege adimu na samaki wa cichlid waliosalia licha ya kuwekwa kwa samaki wa kibiashara kama sangara (Lates niloticus) majini.
Sababu nyingi, ikiwemo uvunaji wa mafunjo (Cyperus papyrus) uliopita kiasi, na kubadilishwa kwa mabwawa kuwa mashamba au maeneo ya ujenzi, sasa zinatishia mfumo huu maalum. Wengi wa wakaazi wanaotegemea mabwawa haya kuwapa riziki wameanza kuwa na wasiwasi kuhusu hatma yake.

Mfumo wa ikolojia unaoinua maisha
Dickson Omondiwao amekuwa akifanya kazi kwenye mabwawa haya yalioko Kaunti ya Kisumu nchini Kenya tangu mwaka 1985. Kila kunapokucha, yeye huingia majini kuvuna mzigo mkubwa wa mafunjo. Anaeleza kuwa kila ifikapo mchana, yeye hushona mikeka, na kukamilisha mitatu kwa siku, kila mmoja ukihitaji takriban mashina 200. Dalali hununua mikeka kutoka kwake na kisha kuiuza sokoni Kisumu. Mikeka hiyo ina matumizi mengi, mara nyingi ikiwa kwenye ujenzi wa kuta.

Fredrick Odhiambo ni msusi wa mikeka na bidhaa nyingine akitumia mafunjo, na anasema yeye na wavunaji wenzake huvuna mashina yaliyokomaa pekee, na kuyaacha yaliyo machanga kumea upya ili bwawa liendelee kujizalisha upya.

Ndani ya mikondo midogo iliyo ndani ya mabwawa haya, wavuvi huweka mitego ya samaki kwa kutumia mashina ya mafunjo. Karibu na bwawa, kwenye maji yaliyo wazi, wavuvi wengine wanaonekana wakitupa nyavu zao. Wao huvua dagaa (Rastrineobola argentea), kambare, tilapia na sangara — pamoja na spishi mpya ambazo zimestawi ziwani.
Ifikapo alasiri, wachimbaji mchanga pia wanajitokeza kwenye mabwawa na kuingia majini. Wanaogelea kwenye maji yanayowafikia kifuani au hata shingoni, huku wakijaza mashua zao kwa mchanga, kisha kutumia fito za mbao kusukuma mashua kurudi kupitia mikondo.


Mashua zilizoelemewa na uzito wa mamia ya kilo za mchanga husukumwa hadi mahali ambapo wamiliki wanasubiri. Malori yanayotoka Kisumu kupitia barabara za udongo zilizochimbika, hufika na wafanyakazi zaidi ambao huyajaza kwa mchanga huo ambao unatumika kwa ujenzi mjini. Mmiliki mmoja wa mashua aliiambia Mongabay: “Hii ndiyo dhahabu yetu ambayo Mungu ametupa.”


Jioni, Emmanuelle Frederick Makokha anaonekana akizungusha wavu wake hewani kabla ya kuutupa mbali, ili kuwanasa samaki. Anasaidiwa na binamu yake ambaye huendesha mashua ya mbao. Wawili hao wanasema mara nyingi wao huvua hadi usiku wa manane.
Kadri giza linavyoingia, wavuvi wengine hula chakula chao cha jioni ufukweni, kabla ya kupanda mashua zao wakiwa kwenye vikundi vya watu watatu au wanne kwa kila moja. Wengi hukaa ziwani usiku kucha, huku wakitandaza nyavu zao zinazoshikiliwa na viboya vinavyoenea mamia ya mita.
Ifikapo alfajiri, mashua hurudi ufukweni, karibu na mabwawa ya mafunjo ya Dunga Beach, ambapo wamiliki wa migahawa, na wafanyabiashara pamoja na wanunuzi wapya wa samaki, huwasubiri.



Hifadhi ya bioanuai
Ziwa Viktoria lilikuwa na mamia ya spishi ya samaki wa cichlid wa haplochromine, kutokana na mchakato wa mageuzi ya kipekee. Lakini mchakato huo ulianguka haraka baada ya kuletwa kwa sangara, ambaye huwinda na kushindana na cichlid wadogo. Karibu na ufukwe, mabwawa ya mafunjo yanaonekana kutoa hifadhi kwa baadhi ya cichlid wa asili.
Utafiti wa Lauren Chapman, ukiwemo uliochapishwa kwenye Biological Conservation na jarida la Fiziolojia, umeonyesha kuwa samaki aina ya cichlid wanapenda mazingira yaliyo na oksijeni ndogo, hasa kwenye mabwawa haya ambayo pia yana msitu mnene wa chini ya maji, ili kujilinda dhidi ya sangara. Mabwawa pia yanaaminika kuwa maeneo ya kuzalia spishi nyingine za samaki, wavuvi wa maeneo ya Ziwa Viktoria wanakiri mchango mkubwa wa mabwawa haya katika kuendeleza sekta ya uvuvi.
Ndani ya mabwawa ya mafunjo, pia kuna spishi nyingi za ndege wa porini wanaostawi katika mazingira maalum ya maziwa makuu barani Afrika.

Mmoja wa ndege maarufu zaidi anajulikana kama papyrus gonolek, ambaye huishi ndani ya vichaka kama hivi, na hujitokeza mara chache sana. BirdLife International limeeleza kuwa gonolek huwa “anapatikana tu kwenye mabwawa ya mafunjo (Cyperus papyrus) na katika mabonde ya mito inayopinda na kandokando ya maziwa.” Tathmini hiyo inaonyesha kuwa idadi ya spishi hii iko kwenye “kupungua kwa kasi ya wastani kutokana na uharibifu unaoendelea na ubadilishaji wa makazi yake ya mabwawa.”
Mabwawa pia ni makazi ya papyrus yellow warbler (Calamonastides gracilirostris), ndege adimu anayepatikana Dunga Swamp karibu na Kisumu. BirdLife International imesema kuwa matumizi ya rasilimali asilia yanachangia kuharibika kwa eneo hili muhimu la ndege.
Licha ya kuhifadhi na kuwapa makao samaki na ndege, mabwawa ya mafunjo huchukua virutubisho kwa kasi na kubakiza mashapo, na hivyo kupunguza mtiririko wao ziwani. Utafiti ambao umechapishwa kwenye Wetlands Ecology & Management umeonyesha kuwa ikiwa katika hali sahihi, C. papyrus inaweza kuchangia kutengenezwa kwa mboji na mabaki yanayoweza kuhifadhi kaboni. Ubadilishaji wa mabwawa kuwa mashamba au maeneo ya ujenzi unaweza kudhoofisha huduma hizi muhimu na kusababisha kupotea kwa bayoanuai.
Lakini tafiti zingine kama ule uliochapishwa kwenye Biological Conservation zinaelezea kuwa “matumizi ya mafunjo kwa kiwango cha chini yanaweza kuendana na uhifadhi wa ndege waliobobea,” hasa kwenye maeneo makubwa ambapo mafunjo yanahifadhiwa. Utafiti huo unaongeza kwamba “uhifadhi wa mabwawa ya kitropiki hauhitaji kutenga kabisa matumizi ya binadamu.”
Mwanasayansi wa mazingira kutoka Kenya, Leonard Akwany, ambaye alianzisha na kuwa mshauri wa Ecofinder Kenya, anasema kuwa uvunaji wa mafunjo unapaswa kufanywa kwa njia ya mpangilio.

Viini vya uharibifu na upotevu
Kwenye mashamba yaliyoko nyuma ya mabwawa, wakulima wanalima mpunga kwenye maeneo yaliyokauka.
Akwany anasema kuna watu ambao huchoma mifunjo ili kufungua njia mpya za uvuvi au nafasi ya kuchimba mchanga. Nicholas Oginga Toya, anayeishi karibu na bwawa, ana wasiwasi kuhusu moto aina hiyo ambao humzuia yeye na familia yake kuvuna mashina. Moto pia umetumika kama hatua ya mwanzo ya kuandaa mabwawa kuwa mashamba.

Kulingana na utafiti wa Nicodemus Osoro Odhiambo, vitisho vya ubadilishaji wa matumizi ya ardhi vinaweza kuwa vikubwa, kama ilivyotokea kati ya mwaka 1990 na 2017, wakati eneo la ardhi oevu la Ombeyi , lililokuwa na karibu hekta 1,000 za mafunjo , na lililokuwa kwenye Kaunti ya Kisumu, lilibadilishwa karibu lote kuwa mashamba na makazi mapya.
Katika miaka ya hivi karibuni, kuna maeneo mengine mapya ya makazi ambayo yamejengwa nyuma ya bwawa kubwa zaidi la mafunjo yaliyoko karibu na Kisumu. Humo ndani ukulima na upandaji wa mboga, pamoja na ufugaji wa vikundi vidogovidogo vya ng’ombe unaendelea.
Udongo kwenye barabara mpya inayotumiwa na wakazi wa nyumba hizo bado unaonekana ukiwa mpya. Wakazi wanasema imejengwa kwenye eneo la bwawa na kwamba nyumba hizo mpya hufurika kila mwaka.

Akwany anataja hoteli na migahawa kadhaa mjini Kisumu iliyojengwa juu ya mabwawa ya mifunjo. Kabla ya kujenga, watu wengi hujaza mawe na udongo ili kuinua ardhi juu ya bwawa. Anasema maeneo hayo ya kitalii, pamoja na ubadilishaji kuwa mashamba, yanaharibu makazi ya mafunjo. Hata hivyo, anasema, kuvuna mafunjo nyakati fulani fulani huleta thamani zaidi kwa bioanuai.
Oginga Toya anakubali kuwa mabwawa pia yana thamani isiyo ya kiuchumi, kwani ni “jambo takatifu,” na kuongeza kuwa, wakati mwingine yeye “huenda na kukaa kimya ndani ya bwawa la mafunjo.” Anasema kuwa kuna roho wanaoishi humo. Wakazi kadhaa wanakubaliana naye, na kusema kuwa maeneo hayo yana umuhimu wa kidini na hutumika kwa ibada.

Akiwa na wasiwasi kuhusu athari za ujenzi unaotishia upatikanaji wa mafunjo, Oginga Toya anasema anatumaini serikali itaweka mipaka. Haijalishi suluhisho litakalopatikana. Wakazi wengi wanahisi maisha yao na riziki zinategemea afya ya mabwawa.
Picha ya bango: Mwanamke akiwa ameshikilia mzigo wa mafunjo yaliyokaushwa na kuandaliwa tayari kwa matumizi. Picha na Patrick B. Newcombe.
Nukuu:
Pringle, R. M. (2005). The origins of the Nile perch in Lake Victoria. BioScience, 55(9), 780-787. doi:10.1641/0006-3568(2005)055[0780:tootnp]2.0.co;2
Pringle, R. M. (2005). The Nile perch in Lake Victoria: Local responses and adaptations. Africa, 75(4), 510-538. doi:10.3366/afr.2005.75.4.510
van Dam, A. A., & Kipkemboi, J. (2018). Sustainable use of papyrus from Lake Victoria, Kenya. In Finlayson, C. M., et al. (Eds.) The Wetland Book (pp. 1113-1124). Springer, Dordrecht. doi:10.1007/978-90-481-9659-3_207
Donaldson, L., Woodhead, A. J., Wilson, R. J., & Maclean, I. M. (2016). Subsistence use of papyrus is compatible with wetland bird conservation. Biological Conservation, 201, 414-422. doi:10.1016/j.biocon.2016.07.036
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 05/02/2024