- Mto Nyamwamba wa Uganda uliokoMilima ya Rwenzori, umeanza kufurika kwa kiwango kikubwa katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
- Kando ya mto kuna mabwawa ya mabaki ya shaba yaliyosalia kwenye shughuli za uchimbaji madini za kampuni ya Canada, ambayo yanazidi kumomonyoka kutokana na mafuriko.
- Kulingana na mfululizo wa tafiti, mabaki haya yamekuwa yakisombwa na maji na udongo wa Bonde la Mto Nyamwamba, na kuchafua tishu za binadamu, chakula na maji kwa metali nzito zenye sumu.
- Viwango vya saratani vimeripotiwa kuwa vya juu kuliko kawaida karibu na mabwawa hayo ya mabaki, na wanasayansi wanahofia kwamba mafuriko yanapoendelea kuwa mabaya, ndivyo pia shida ya kiafya itakavyoongezeka.
Hii ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala kuhusu majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya Magharibi mwa Uganda. Soma Sehemu ya Kwanza hapa.
KASESE, Uganda – Mara tu Mto Nyamwamba unapopita katika miteremko ya Milima ya Rwenzori magharibi mwa Uganda, na hatimaye kuanza kutiririka kuelekea kwenye savanna, unapita kwenye eneo la kushangaza. Katika upande wa pili wa mto kutoka barabarani, hupita marundo ya mawe yaliyopauka kwa jua kwenye mto uliokauka, ardhi iliyoharibiwa. Kuta ndefu zinasimama wazi, zikichomoza katikati ya vilima, kana kwamba mkono wenye nguvu umechukua sehemu ya mandhari hiyo. Miamba mikali huchomoza ghafla kutoka kwenye vichaka vya kijani juu, ikishuka hadi kwenye shimo tambarare la mchanga na mawe ya rangi ya hudhurungi.
Hili ni bwawa la mabaki ya shaba. Pamoja na mabwawa mingine, linatia sumu kwenye sehemu hii ya Uganda.
Mabwawa hayo yalijengwa kuhifadhi taka kutoka kwenye mgodi wa shamba uliokuwa unamilikiwa na Falconbridge, kampuni ya Canada ambayo iliendesha shughuli zake katika miteremko ya Milima ya Rwenzori kuanzia miaka ya 1950 hadi mwishoni mwa miaka ya 1970. Wakati wa enzi zake, mgodi wa shaba wa Falconbridge, ulioko kando ya barabara katika mji mdogo wa Kilembe, ulikuwa injini kuu ya uchumi wa Uganda. Mgodi huo uliwahi kuajiri zaidi ya watu 6,000 na ulichangia karibu theluthi moja ya Pato la Taifa.
Falconbridge ilifukuzwa nchini Uganda na Idi Amin mwaka 1977, ambaye alitaifisha mgodi huo katika miaka ya mwisho ya utawala wake, akiwa na imani kwamba serikali yake inaweza kuuendesha pamoja na Wakanada na kuweka thamani zaidi ya shaba nyumbani. Kufikia mwaka 1982, ulifungwa.
Huko Kilembe, mizimu ya Falconbridge inapatikana kila mahali. Nyumba ya kampuni iliyooza bado inamilikiwa na wafanyakazi wa zamani na vizazi vyao. Miundombinu mibaya ya uchimbaji madini iko kwenye mlima. Mabwawa ya mabakii ya shaba yamesalia kama ukumbusho wa kile ambacho hapo awali kilichukuliwa kutoka hapa na kupelekwa kaskazini ili kuendeleleza mashine za uchumi wa mataifa ya magharibi katika kipindi cha enzi za ubepari.

Urithi wa sumu sasa unatiririka kutoka kwenye madimbwi haya na kuingia kwenye maji, udongo na miili ya watu wa eneo katika eneo hili, huku Mto Nyamwamba ukiendelea kupasua kingo zake kwa kasi. Ongezeko la joto duniani limeathiri hali ya hewa juu ya milima – wakati wa msimu wa mvua, mafuriko yamekuwa ya kawaida zaidi. Maji ya mafuriko ya Mto Nyamwamba yanapozidi kupita karibu na mabwawa haya kila mwaka, vyuma vizito vyenye sumu vinasombwa na kuelekea mji mkuu wa wilaya ya Kasese ambako kuna wakazi wapatao 100,000.
Huko Kilembe, athari tayari zinaonekana wazi. Viwango vya saratani vimeongezeka sana. Kwa kuchochewa na uchomaji wa mafuta katika maeneo ya mbali, majeraha ya uchimbaji madini katika eneo hili yameanza kuonekana na kuwa mabaya zaidi kama vidonda vinavyozidi kuambukizwa.
“Tulipokuwa tukianzisha utafiti wetu katika eneo la mgodi wa Kilembe, dampo (hili) lote la mabaki halikuguswa na maji,” alisema Abraham Mwesigye, mwanasayansi wa mazingira katika Chuo Kikuu cha Makerere cha Kampala. “Lakini kwa sababu ya mafuriko, tumepoteza tani na tani za taka kwenye Mto Nyamwamba … na hiyo imetokea tu katika miaka minne iliyopita wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zilipoongezeka katika Milima ya Rwenzori.”

Madimbwi ya hatari
Kwa jumla, kuna tani milioni 15 za mabaki ya shaba katika eneo linalozunguka Kilembe. Muongo mmoja uliopita, Mwesigye na wenzake walianza kuchunguza athari za mabaki hayo kwa afya na mazingira. Katika kipindi hicho, tafiti baada ya tafiti zimeonyesha matokeo ya kushangaza.
Shaba, kobalti, arseniki, nikeli, zinki na risasi vipo kila mahali. Kuna nikeli kwenye mihogo na maharage yanayopandwa kando ya kingo za Mto Nyamwamba. Mkusanyiko wa shaba ni mara kadhaa zaidi kuliko wastani katika kucha za miguu ya watu. Kwenye zaidi ya nusu ya sampuli zilizochukuliwa za maji ya kunywa karibu na Kilembe na chini ya mto mwaka 2017, kulikuwa na viwango visivyo salama vya chuma aina ya kobalti. Udongo umechafuliwa, vumbi linalopatikana ndani ya nyumba za watu ni sumu, na hata nyasi zinazoliwa na mifugo na wanyama wa mwitu zinaonyesha uwepo mkubwa wa metali nzito.
Viwango hivi vya sumu ni vya juu zaidi, na mara nyingi ni hatari, hasa karibu na eneo la Kilembe. Lakini pia zinaweza kupatikana chini ya mto, karibu na mji wenye watu wengi zaidi wa Kasese.
“Mara nyingi taka hizi zimekuwa zikisombwa hadi kwenye mashamba na Mto Nyamwamba, ambao ni chanzo kikuu cha maji kwa wenyeji,” Mwesigye alisema katika mahojiano ya simu na Mongabay. “Hatari ni kwamba zina vyuma vizito, vikiwemo vyenye sumu kali. Tunazungumzia shaba, kobalti, zinki, arseniki, manganizi na chuma. Tulipima na tukagundua zaidi ya aina 42 kwenye taka hizo, ambazo zinaishia kwenye vyanzo vya maji ya kunywa na ya kilimo.”

Baadhi ya elementi zinazoingia kwenye Mto Nyamwamba zinasababisha kansa. Kobalti, kwa mfano, hivi majuzi iliorodheshwa na Tume ya Ulaya kama yenye kiwango cha hatari cha daraja 1B, ikimaanisha kuwa ikimfikia mtu kwa kiwango kikubwa, kuna uwezekano wa kumsababishia saratani. Sampuli za viazi vikuu vilivyolimwa karibu na Kilembe mnamo mwaka 2019 zilionyesha viwango vya kobalti ambavyo vilizidi kiwango cha usalama hasa kwa watoto .
“Kobalti ni ya pili kwa kuwa na sumu nyingi katika eneo la Kilembe baada ya shaba,” alisema Mwesigye.
Sumu hizi zinasababisha matatizo ya kiafya yasiyoonekana wazi lakini ambayo yanaongezeka kwa kasi huko Kilembe, aliongeza.
“Tulifanya utafiti katika hospitali na vituo vya afya vya Kilembe, na tukagundua kuwa kuna viwango vya juu vya saratani na magonjwa ya mfumo wa kumeng’enya chakula , ambayo yote yanahusishwa na athari za kuathiriwa na sumu hizo.”
Hadi sasa hakujafanyika tafiti za uhakika zinazohusisha moja kwa moja kuenea kwa vyuma vizito huko Kilembe na Kasese na ongezeko la viwango vya juu vya saratani. Lakini ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa viwango hivi ni vya juu kuliko wastani ikilinganishwa na maeneo mengine ya Uganda. Maafisa wa manispaa ya Kasese wanasema wanahisi kuwa madimbwi ya mabaki ya shaba ndiyo chanzo, kwa sababu sumu zimeanza kuonekana kwenye mazao ambayo watu wanakula.
“Tunafikiria kwamba ongezeko la saratani katika eneo hili linaweza kwa kiasi fulani limesababishwa na maji yanayotumika kukuza mazao ya chakula,” alisema Chance Kahindo, Meya wa Kasese.
Matokeo ya Mwesigye yameungwa mkono na watafiti wengine. Katika utafiti wa mwaka 2020 uliochapishwa katika Jarida la Octa la Utafiti wa Mazingira, sampuli zilizochukuliwa kutoka kwenye Mto Nyamwamba karibu na Kilembe zilionyesha kuwa na viwango vya shaba na kobalti ambavyo vilivuka mipaka salama iliyowekwa na Shirika la Afya Ulimwenguni. Sampuli za tishu zilizochukuliwa kutoka kwa samaki wa mto huo, ukiwa ni chanzo muhimu cha chakula kwa wenyeji, pia zilirekodiwa kuwa zilikusanya kiasi kisicho salama cha kobalti, risasi na zinki.
Watetezi wa mazingira wanasema kwamba kuna uwezekano mkubwa kuwa madini hayo pia yanaathiri wanyamapori katika Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth, hifadhi kubwa ya asili ambayo Mto Nyamwamba hukatiza ukiingia Ziwa George. Likiwa eneo la Urithi wa Dunia la UNESCO, mbuga hiyo ni makazi ya simba, nyati, chui, viboko na tembo wa savanna ya Afrika.
“Mabaki haya ya shaba yanaishia kwenye maji,” alisema Edwin Mumbere, mkurugenzi wa kikundi cha mazingira chenye makao yake makuu kwenye mji wa Kasese. “Kwa hivyo kuna uchafuzi wa metali nzito ambazo haziathiri sisi tu kama jamii, bali pia wanyama walioko katika mbuga.”


Hata kufikia mwaka wa 2003, utafiti ulionyesha viwango vya juu kuliko kawaida vya shaba na zinki katika Ziwa George, takriban kilomita 30 (maili 19) chini ya Mto Kilembe, ikiwa ni pamoja na samaki wanaolisha makumi ya maelfu ya watu katika eneo hilo. Viwango vilivyogunduliwa katika miili yao vilionekana kuwa salama kwa matumizi ya binadamu – lakini hiyo ilikuwa kabla ya mafuriko ya Mto Nyamwamba kuanza kuwa mabaya zaidi na ya mara kwa mara.
Mwaka 2022, mtafiti wa Taasisi ya Saratani ya Uganda alimwambia mwandishi wa habari kwamba matukio ya saratani kutoka Kasese “yanaonekana kuongezeka,” lakini uhusiano kati ya matatizo ya afya katika eneo hilo na kuenea kwa metali nzito haujachunguzwa kikamilifu. Kulingana na data ambazo hazijachapishwa rasmi na ambazo zimesharekodiwa na Mongabay na Taasisi ya Saratani ya Uganda yenye makao yake makuu Kampala, utafiti wa hivi majuzi haukuonyesha viwango vya juu kuliko wastani vya saratani katika wilaya ya Kasese kwa ujumla. Lakini takwimu hizo zilijumuisha idadi kamili ya wakazi 800,000 wa wilaya hiyo, na hazikuwa zimegawanywa ili kuchambua viwango vya saratani kwa watu wanaoishi katika mji wa Kasese au makazi mengine yaliyo kati ya Kilembe na Ziwa George.
“Mazao ya chakula yanayolimwa Kilembe yanauzwa katika mji mzima wa Kasese,” Mwesigye alisema. “Kwa hiyo kuna uwezekano kwamba wakazi wa Kasese wanakula vyakula vilivyochafuliwa … na kunapokuwa na mafuriko, unakuta mabaki huko, kwa sababu Mto Nyamwamba huvunja kingo zake na kusambaza taka kila mahali.”
Kwa watu katika eneo hili ambao wanaathiriwa na saratani, kokote inakotoka, mara nyingi hukumbwa na mateso makubwa. Ikiwa hawana pesa za kulipia matibabu katika moja ya wodi maalum za kibinafsi za Kampala, hakuna wanachoweza kufanya zaidi ya kusubiri ugonjwa huo kuwaangamiza. Ripoti za vyombo vya habari zinazungumza juu ya wagonjwa waliopatwa na maradhi hayo wakifa taratibu majumbani mwao bila kupata matibabu sahihi.

Makovu ya zamani yamefunguliwa na majeraha mapya
Sumu zinazopita katika mifumo ya uhai ya Kilembe zimezalisha janga ambalo ni la dharura, na angalau kwa sasa, limekuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Hakuna chaguo: hata maji yanapoongezeka na sumu huingia ndani zaidi kila mwaka, watu wanaoishi kando kando ya Mto Nyamwamba wanalazimika kuzoea hali hiyo. Hali hii siyo tatizo lenye upekee. Kadri ikolojia inavyobadilika na gharama za maendeleo ya karne ya 20 zinavyozidi, watu walio karibu mara nyingi hawana chaguo lolote zaidi ya kujaribu kulitafutia ufumbuzi.
Barani Afrika kote na vile vile katika maeneo mengine ambayo misitu na migodi yake ilikuza uchumi wa dunia, kuna majeraha, yaliyoachwa na yanayoendelea kuvuja damu hata baada ya mikono iliyoyafungua kutoweka kwa muda mrefu.
“Bado tuko katika awamu ya uchimbaji katika nchi za Amerika ya Kusini na Afrika, lakini tatizo litajitokeza katika karne ijayo wakati zitakapobaki athari za kile kilichofanyika,” alisema Flaviano Bianchini, Mkurugenzi wa Shirika la Source International, shirika lisilo la kiserikali ambalo linafanya kampeni kwa niaba ya jamii zilizoathiriwa na madini. “Gharama ya kusafisha uchafuzi unaosababishwa na mgodi ni kubwa, kubwa sana. Ni mamilioni na mamilioni ya dola.”
Barani Afrika, athari hizi tayari zimeshamiri. Katika taifa jirani laJamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mgodi wa shaba unaomilikiwa na kampuni ya kimataifa ya Glencore ya Uswizi katika jimbo la Lualaba, umeifanya ardhi isiwe katika hali ya kuweza kutumika na kuharibu vyanzo vya maji vya wakazi wa eneo hilo. Mwaka 2022, kampuni hiyo ilikubali kulipa dola za Marekani milioni 180 kwa nchi hiyo baada ya kukiri kwamba ilitumia zaidi ya muongo mmoja kuwahonga maafisa wakuu huko.
Kusini zaidi, katika taifa la Zambia, watoto waliozaliwa katika mji wa Kabwe, ambao ulikuwa na mgodi wa risasi unaoendeshwa na kampuni ya kimataifa ya Uingereza, Anglo-American, kati ya miaka 1925 na 1974, wanaweza kuwa na viwango vya risasi katika damu mara 20 zaidi ya kiwango salama. Kilembe si mji wa nje – ni kawaida.

Baadhi ya mawakili wa maslahi ya umma wanajaribu kubadilisha hali hiyo na kuyawajibisha makampuni. Lakini wanakabiliwa na vita kubwa. Mnamo Desemba, mahakama ya Afrika Kusini ilitupilia mbali kesi ambayo kampuni yenye makao yake makuu nchini Uingereza Leigh Day ilifungua dhidi ya Anglo-American kuhusu uharibifu iliyoacha huko Kabwe.
Mahakama ilisema kwamba kwa kujaribu kulazimisha Anglo-American kulipia uharibifu, walalamikaji walitaka “kuendeleza madai yasiyoweza kutekelezeka ambayo yangeweka mfano mbaya.”
Wakati kampuni ya Leigh Day ikiendelea na mchakato wa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, kitendo hicho kinaashiria matatizo ambayo jamii hukabiliana nayo katika mahakama za Afrika wanapokabiliana na makampuni makubwa ya madini au serikali. Kutojali kumesababisha madhara.
“Linapokuja suala la madhara ambayo yamekuwa yakiwaathiri wafanyakazi na jamii, ukosefu wa upatikanaji wa haki ndani ya nchi umesababisha kukosekana kwa nidhani na motisha ya kutosha kwa makampuni kufanya vyema,” alisema Richard Meeran, Wakili Mkuu kutoka kampuni ya Leigh Day kuhusu kesi ya Kabwe.
Wakati makampuni yanapomaliza shughuli zake na kuondoka, iwe kwa sababu mgodi umepungua, uendeshaji hauwezi tena kumudu gharama, au kutokana na mgogoro na serikali, ni watu wanaoishi karibu – wale walio na rasilimali ndogo – wanaobaki kubeba mzigo wa dharama na madhara yaliyosalia.
“Mifumo ya kisheria sharti ibadilike ili kuwajibisha makampuni,” alisema Marcos Orellana, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu sumu na haki za binadamu, katika barua pepe aliyoituma kwa Mongabay. “Na mahakama lazima ziwe wazi na tayari kuwawajibisha wachafuzi wa mazingira waliopita kwa madhara ambayo wamesababisha kwa jamii na mazingira.”
Haitasaidia sana kwa mtu yeyote anayeishi Kilembe au Kasese kubisha hodi kwenye mlango wa kampuni ya Falconbridge. Mnamo mwaka 2006, ilinunuliwa na kampuni ya Uswizi-Anglo Xstrata, kwa makubaliano ya dola za Marekani bilioni $ 22.5 ambayo ilikuwa moja ya makubaliano makubwa zaidi katika historia ya Canada wakati huo. Miaka michache baadaye, kampuni ya Xstrata ilinunuliwa na Glencore, kampuni kubwa zaidi duniani ya bidhaa za malighafi. Kulingana na data ya kampuni, mnamo mwaka 2022 kampuni ya Glencore ilipata faida ya kihistoria ya dola za Marekani bilioni 17.3, na ikalipa zaidi ya dola za Marekani bilioni 7 kwa wanahisa wake.
Katika barua pepe kwa Mongabay, kampuni ya Glencore ilikataa kutoa maoni yake kuhusu urithi wa kampuni ya Falconbridge nchini Uganda.

Licha ya athari zake mbaya, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ametumia muda wa muongo mmoja kujaribu kuanzisha upya uchimbaji wa shaba huko Kilembe. Baada ya tukio la aibu ambapo kampuni ya China iliudhibiti mgodi huo na kupoteza kandarasi yake kutokana na kutofanya kazi na kutolipwa ada, serikali ya Uganda imepata wawekezaji wapya. Mwishoni mwa mwaka jana, mji wa Kilembe ulikuwa mwenyeji wa ujumbe wa kuonyesha miundombinu iliyoachwa na kampuni ya Falconbridge. Ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha mpango mpya unaweza kuwa unakaribia.
Iwapo mmiliki mpya atapatikana, haijulikani ni nini, kama kutakuwa na chochote, atafanya kuhusu mabwawa ya mabaki na urithi wao mbaya.
Kwamba majeraha ya mazingira kutoka kwa siku za usoni zinazokaribia kwa kasi yanachanganyika na yale ya historia isiyotatulika ya magharibi mwa Uganda, kunatoa ujumbe mzito. Mgogoro wa tabianchi hauji peke yake. Utakuja na wenza wake.
Wakati huo huo, watu wanaoishi kandokando ya Mto Nyamwamba wanakabiliwa na migogoro miwili ya kiikolojia kwa wakati mmoja, tofauti lakini yenye uhusiano. Kutoka juu, anga linalozidi kuwa na joto inawanyang’anya maeneo yao matakatifu na kuwafukuza kwenye nyumba zao kupitia mafuriko makubwa. Wakati huo huo, sumu kutoka kwenye ardhi iliyo na makovu hupenya zaidi kwenye chakula chao, maji na miili yao. Kutoka pande zote mbili ni madhara ya uchimbaji, na hakuna nafuu inayoonekana.
Majeraha ya kimazingira yanayotarajiwa siku za usoni zinazokaribia kwa kasi yanayoambatana na yale ya zamani ambayo hayajatatuliwa ya Magharibi mwa Uganda, yana ujumbe wa kutisha. Mgogoro wa tabianchi hauji peke yake. Utakuwa na mwenzake.
Picha ya bango: Viboko katika Mbuga ya Taifa ya Malkia Elizabeth. Watetezi wa mazingira wanasema kuna uwezekano mkubwa kwamba madini hayo pia yanaathiri wanyamapori katika mbuga hiyo. Picha na Ashoka Mukpo/Mongabay.
Eric Mwesige alichangia ripoti hii kutoka Kasese, Uganda.
Nukuu:
Owor, M., Hartwig, T., Muwanga, A., Zachmann, D., & Pohl, W. (2006). Impact of tailings from the Kilembe copper mining district on Lake George, Uganda. Environmental Geology, 51(6), 1065-1075. doi:10.1007/s00254-006-0398-7
Mwesigye, A. R., & Tumwebaze, S. B. (2017). Water contamination with heavy metals and trace elements from Kilembe copper mine and tailing sites in western Uganda; Implications for domestic water quality. Chemosphere, 169, 281-287. doi:10.1016/j.chemosphere.2016.11.077
Mwesigye, A. R., Young, S. D., Bailey, E. H., & Tumwebaze, S. B. (2019). Uptake of trace elements by food crops grown within the Kilembe copper mine catchment, Western Uganda. Journal of Geochemical Exploration, 207, 106377. doi:10.1016/j.gexplo.2019.106377
Mwesigye, A. R., Young, S. D., Bailey, E. H., & Tumwebaze, S. B. (2016). Population exposure to trace elements in the Kilembe copper mine area, Western Uganda: A pilot study. Science of The Total Environment, 573, 366-375. doi:10.1016/j.scitotenv.2016.08.125
Masereka, J., Byamugisha, D., & Adaku, C. (2022). Heavy metal accumulation in vegetables grown in rock soils of Kilembe copper mine, Kasese, Western Uganda. Asian Journal of Applied Chemistry Research, 30-40. doi:10.9734/ajacr/2022/v12i1213
Mukisa, W., Yatuha, J., Andama, M., & Kasangaki, A. (2020). Heavy metal pollution in the main rivers of Rwenzori region, Kasese district south-western Uganda. Octa Journal of Environmental Research, 8(3), 78-90. Retrieved from http://sciencebeingjournal.com/sites/default/files/02_0803_MW01.pdf
Swaibuh Lwanga, M., Kansiime, F., Denny, P., & Scullion, J. (2003). Heavy metals in Lake George, Uganda, with relation to metal concentrations in tissues of common fish species. Hydrobiologia, 499, 83-93. doi:10.1023/A:1026347703129
Balasha, A. M., & Peša, I. (2023). “They polluted our cropfields and our rivers, they killed us”: Farmers’ complaints about mining pollution in the Katangese Copperbelt. Heliyon, 9(4), e14995. doi:10.1016/j.heliyon. 2023.e14995
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 06/03/2024