- Nchini Kenya, kilimo kidogo na ufugaji wa samaki ufukweni pamoja na mbinu endelevu za kilimo-ikolojia kinakuza usalama wa chakula na kipato kwa wakulima wadogo.
- Ingawa idadi kubwa ya mashamba haya ni madogo sana, kiasi kikubwa cha protini kinaweza kukuzwa katika mabwawa ya samaki yaliyojaa maji ya mvua.
- Wakilishwa na mchanganyiko wa taka za chakula na mabaki ya mazao kutoka kwa kilimo mseto na kilimo-hai, samaki kama tilapia wanaweza kufugwa kwa njia endelevu na kwa faida.
- Kaunti tisa zimewekeza katika kusaidia miradi kama hiyo ya ufugaji samaki, huku katika eneo la Gatunga, sehemu ya kati ya Kenya pekee, kukiwa na takribani wafugaji 300 wa samaki.
GATUNGA, Kenya — Msimu wa ukame ambao uliisumbua Kenya kwa miaka michache iliyopita umetikisa mifumo ya chakula vijijini nchini humo. Lakini Japheth Nthiga, mkulima kutoka kijiji cha Karethani sehemu ya kati ya Kenya, amekuwa akipata faraja wakati wa kipindi kigumu.
Hiyo ni kwa sababu Nthiga amebadilisha sehemu ya ardhi yake kuwa mabwawa ya kufugia samaki, huku shamba lake lililosalia, likisaidia mifugo na mazao ya chakula kama maharage ya kijani, mtama, uwele na mahindi. Tangu mwaka 2013, ni nusu ekari tu ya eneo lake ambayo imemnufaisha zaidi.
“Samaki ninaowafuga hapa ni kwa ajili ya matumizi ya ndani. Pia ninapata mapato mazuri ninapouza samaki katika soko la huku nchini. Sioni wasiwasi wakati mazao yangu ya chakula yanaposhindwa kutoa mavuno,” alisema baba huyo wa watoto watano mwenye umri wa miaka 51, anayefuga ngege na kambare.

Ni rahisi kuelewa vizuri hisia za Nthiga. Kijiji chake, ambacho kiko takriban kilomita 150 (sawa na maili 90) kutoka ukingo wa Msitu wa Mlima Kenya, kimekumbwa na ukame wa muda mrefu na wa mara kwa mara kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Ili kukabiliana na msimu wa kiangazi, wakulima, hasa wale wanaotoka katika nyanda za juu za mito, wamezidisha matumizi yao ya mbolea ili kuongeza mavuno, na kwa kufanya hivyo, wamesababisha uchafuzi wa mito na kupoteza rutuba ya udongo katika eneo hilo, kulingana na Venter Mwongera, ambaye ni mratibu wa mawasiliano na utetezi katika shirika la Biodiversity Africa.
Matokeo yake, mifumo ya chakula vijijini inakabiliwa na vitisho vya kupungua kwa mavuno, Mwongera alisema.
“Kemikali za kilimo zinatia sumu kwenye mifumo ya vyakula barani Afrika, lakini wakulima wachache wanafahamu kuwa wanaagiza tatizo hili kutoka kwa mabara tajiri zaidi. Kukubali kilimo ikolojia kwa uhuru wa chakula ndio ulinzi wa mwisho wa bara hili dhidi ya tishio hili,” alisema.
Kilimo ikolojia ni neno la mifumo inayoongeza mavuno ya kilimo huku ikipunguza uharibifu wa mazingira kupitia mazoea kama vile kilimo-hai. Ufugaji wa samaki ufukweni unaweza kuwa mojawapo ya mazoea hayo.
Hii ni kwa sababu haihitaji uwekaji wa kemikali hatari za kilimo kama vile mbolea ya usanisi. Kinachohitajika ni upatikanaji wa maji ya kutosha na mapenzi kwa kilimo hicho, Mwongera aliiambia Mongabay.

Ufugaji wa samaki wazidi hupata umaarufu
Mabwawa mawili ya samaki ya Nthiga yaliyotunzwa vyema huwavutia wageni kufika kwake. Wengine huja kujifunza kilimo cha ufugaji samaki, wakiwemo wanafunzi kutoka ukanda huo wanaofanya kazi kwenye miradi yao ya utafiti. Wengine wanakuja kununua samaki moja kwa moja kutoka kwenye chanzo, huku wengine wakija kupata mlo wa samaki waliopikwa kutoka nyumbani kwake, alisema.
“Tangu nianze mradi huu wa ufugaji wa samati, kila wakati nakuwa na shughuli nyingi. Nina furaha kuwa ninawahamasisha wakulima wengine kuelekeza juhudi zao katika kilimo hiki cha samaki,” alisema na kuongeza kuwa sasa kuna wafugaji sita katika kijiji chake ambao walifuata maelekezo yake, ingawa eneo kubwa la Gatunga lina zaidi ya wafugaji 300.
Hakuna rekodi rasmi kuhusu ni Wakenya wangapi wanafanya kilimo kidogo cha kufuga samaki nchini. Lakini kufikia mwishoni mwa mwaka 2022, kaunti tisa tayari zilikuwa zimewekeza kusaidia ufugaji samaki, kulingana na Micheni Ntiba, aliyekuwa katibu mkuu wa idara ya kitaifa ya uvuvi.
Nthiga anatoka katika mojawapo ya kaunti hizi, na ni miongoni mwa watu wa kwanza kuwekeza binafsi katika ufugaji wa samaki, na hivyo kuthibitisha kuwa sehemu kubwa ya Kenya inafaa kwa ufugaji wa samaki katika nchi kavu, kama vile Ntiba alivyosema kwenye mkutano wa hadhara wa mwaka 2022 na wakulima sehemu ya kati ya Kenya.
Nthiga huvuna maji ya mvua kutoka kwenye mfumo wa kukusanya kupitia paa la nyumba ili kujaza mabwawa hayo, ambayo yameezekwa na mifuko ya plastiki migumu ili kuzuia upotevu wa maji. Nthiga pia hupokea maji kutoka kwa mradi wa umwagiliaji wa kijiji hicho.
John Macharia, mratibu wa kitaifa wa mpango wa Kilimo Endelevu kwa Shule na Vyuo yaani (SCOPE-Kenya), alisema ufugaji wa samaki katika nchi kavu nchini Kenya unasaidiwa na kilimo cha kudumu, mfumo wa kilimo unaotumia mbinu za asili kufanya kilimo chenye kurejesha uhai wa ardhi kikizingatia utofauti wa mazao, ustahimilivu, uzalishaji wa kiasilia na uendelevu.
Kwa mfano, alisema mfumo huo unategemea uvunaji wa maji ili kuhudumia mashamba ya kilimo cha samaki. Pia huingia kwenye kilimo cha miti ili kutoa kivuli kwa mabwawa na kuwapa samaki chakula cha jioni wakati baadhi ya miti hii inapodondosha majani yanayoweza kuliwa kwenye maji.

Kutafuta chakula cha samaki
Utekelezaji wa kilimo mseto, unaojumuisha matunda, malisho na miti muhimu ya mbao katika mifumo ya kilimo, limekuwa jambo rahisi kwa wakulima wengi wadogo wadogo kama Nthiga. Lakini wakati wa kulisha samaki, mambo yanakuwa ghali kidogo.
Hii ni kwa sababu samaki wanahitaji chakula chenye protini nyingi, kiungo ambacho kawaida yake hutolewa katika mfumo wa tembe za chakula zinazouzwa katika maduka ya rejareja sehemu za vijijini ili kuhifadhi chakula cha mifugo. Vidonge vya chakula cha samaki ni ghali kwa wakulima wadogo (na si endelevu vinapotengenezwa kutoka kwa samaki hatari wa pwani, ngisi na kamba), lakini shirika la SCOPE-Kenya limewafundisha wakulima mbinu chache za kupambana na changamoto hiyo.
“Baadhi ya wakulima hurudisha mabaki ya chakula kutoka kwa milo ya familia na pia hutumia mboga kutoka kwenye bustani zao za mboga kulisha samaki. Wengine wanakuza mwani ndani ya mabwawa, ambayo inaweza kutumika kama chakula na kuongeza oksijeni kwa samaki,” Macharia alisema.
Nyumbani kwake Nthiga, chakula cha jioni cha samaki hao hutolewa zaidi kutoka shambani mwake kwa kukusanya makapi ya mahindi, kunde, alizeti na keki ya pamba, pamoja na damu inayofyonzwa na kukamuliwa kutoka kwa mifugo iliyochinjwa kwenye mabucha ya kienyeji.
Kisha baadaye husafisha viungo vya mmea na kutibu damu ya mnyama kwa maji ya moto ili kuua bakteria na virusi, kisha huvichanganya pamoja. Baada ya kupeleka mchanganyiko huu katika mashine ya kienyeji ya kusaga, yeye huongeza glasi mbili za kunywea za unga wa ngano au glasi tatu za unga wa muhogo, na maji ili kukilainisha.

Hii inatayarisha mchanganyiko ambao huchakatwa na kuwa mikunjo myembamba na kutandazwa chini ya kivuli ili kukauka. Na Mara inapokaushwa, Nthiga hukata makungu kuwa vidonge vya samaki.
“Mimi pia huwalisha samaki kwa mkate, wali na mabaki mengine ya kutoka jikoni. Kupitia njia hii, mimi huhakikisha hakuna uharibifu wa vyakula nyumbani kwangu,” alisema.
Stakabadhi ya kazi kutoka kwa Shirika la Muungano wa Uhuru wa Chakula Barani Afrika (AFSA) ilisema ufugaji wa samaki unahimiza kilimo mseto, pia, ukuzaji wa miti kwa kuwa maji ya kufugia samaki hutumika kumwagilia miti hiyo, ambayo husaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuunda hali ya hewa ndogo.
Million Belay, mratibu mkuu wa shirika la AFSA, alisema ikiwa itafanywa ipasavyo, mifumo hii ya kilimo cha miti asilia pia inabuni mazingira ya kuvutia nyuki, ndege, wanyamapori na vijidudu.
Viumbe hawa wote wanaweza kusaidia mifumo ya vyakula barani Afrika, ambayo imerekodi mapungufu katika uwezo wa uzalishaji wa chakula kwa kati ya asilimia 10 hadi asilimia 20. Wakati huohuo, asilimia 13 ya ardhi ya kilimo imepotea kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, alisema.
“Kilimo ikolojia kinaweza kuipa Afrika lishe, afya, mazingira na ulinzi wa bayoanuwai pamoja na kuongeza uzalishaji wa chakula. Hii ni kwa sababu mfumo huo unatokana na ujuzi na utamaduni wa watu,” Belay alisema.
Hata hivyo, ili mifumo ya kilimo cha kudumu kama hii ifanikiwe, ni sharti ifanye kazi na asili na sio dhidi yake, pamoja na kuweka mawazo juu ya suluhisho na sio shida, Macharia alisema.

Nthiga amevifanyia kazi vidokezo hivi na amefurahishwa na matokeo yake. Hivi majuzi ameona aina mpya ya ndege wakiwa kwenye miti yake, huku wanyamapori wengine kama nungu wakianza kurejea kijijini mwake. Na huku misitu katika shamba lake ikimpatia kuni, matunda na mitishamba, ongezeko la idadi ya nyuki linakuza uzalishaji wa asali katika mizinga ambayo anaikita kwenye miti.
Lakini safu ya fedha haipaswi kuficha wingu: mafanikio ya biashara yake ya ufugaji wa samaki pia yamevutia wanyama wanaowinda. Chatu wa miamba ya Kiafrika ambao hufika kwenye madimbwi ili kupunguza kiu yao, wakati mwingine hushambulia mifugo yake. Kasa, ndege wa usiku na mtilili pia huwinda samaki wake na wanaweza kusafisha hata bwawa zima lililojaa. Lakini mbaya zaidi ni mabungo ya kwenye maji, ambayo wakati mwingine huvamia kundi kubwa mwanzo wa msimu wa mvua. Wadudu hao hula nyama ya ndani ya samaki wachanga, samaki wadogo wenye urefu wa sentimeta 10 hadi 15 (sawa na inchi 4-6) na kuacha uchafu unaoelea wa mabaki yaliyokufa.
Kwa sababu kilimo cha Kenya ni aina ya kilimo cha wakulima wadogo wadogo ambacho kinafanywa katika mashamba ya ukubwa wa wastani wa hekta 0.2-3 (sawa na ekari 0.5-7.4), huku sehemu kubwa ya chakula kinachozalishwa kwa ajili ya kujikimu, kuna haja kubwa ya kuongeza usambazaji wa chakula ili kukidhi mahitaji: wakulima wadogo wanachangia takriban asilimia 70 ya jumla ya uzalishaji wa kilimo, na kukidhi takriban asilimia 75 ya mahitaji ya kitaifa ya chakula.
Je, mabwawa ya samaki yanaweza kutoa sehemu ya jibu la pengo lililoko ?
“Kuna wakulima zaidi kama mimi wanaoweza kuimarisha hifadhi ya chakula na lishe nchini Kenya. Lakini tunahitaji usaidizi katika suala la kupata samaki wachanga bora na maeneo yao ya kuzaliana karibu na mashamba yetu,” alisema Nthiga, ambaye ana mpango wa kujenga eneo lake la kuzaliana samaki wadogo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Picha ya bango: Samaki aina ya ngege wakiwa katika bwawa la samaki linalomilikiwa na Japheth Nthiga, mkulima kutoka kijiji cha Karethani sehemu ya kati ya Kenya. Picha na David Njagi wa Mongabay.
Nukuu:
HLPE (2019). Agroecology and other innovative approaches for sustainable agriculture and food systems that enhance food security and nutrition. High Level Panel of Experts on Food Security and Nutrition of the Committee on World Food Security, Rome. Retrieved from https://www.fao.org/3/ca5602en/ca5602en.pdf
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 08/02/2023