- Sensa ya wanyama iliyofanyika hivi karibuni inaonyesha kuwa idadi ya nyani aina ya Kipunji (Rungwecebus kipunji) wanaopatikana Nyanda za Juu Kusini nchini Tanzania wameongezeka kwa asilimia 65. Kwa upande mwingine uharibifu wa makazi yao kutokana na shughuli za binadamu umepungua kwa asilimia 81 kwa kipindi cha miaka 13.
- Mafanikio haya yanatokana na jitihada za miaka 20 ya uhifadhi jumuishi unaofanywa na Shirika la Kuhifadhi Wanyamapori, serikali ya Tanzania na washirika wa serikali, ukiwemo usimazi thabiti wa sheria za misitu na ushirikiano na jamii.
- Jamii ya kipunji inakadiriwa kuwa na wanyama 1,966 wakiwa katika makundi mawili na kulingana na shirika la kimataifa la IUCN,wanyama hao wako hatarini kutoweka.
- Kipunji wamejumuishwa katika orodha ya wanyama ambao wamo hatarini kutoweka, orodha inayojumuisha aina 25 za nyani. Orodha hiyo imechapishwa katika vipidi tofauti vya mwaka 2006-2008, 2008-2010, na 2018-2020, lakini kipunji hawamo katika orodha ya hivi karibuni.
Mnamo Januari 2003, watafiti kutoka Shirika la Kuhifadhi Wanyamapori (Wildlife Conservation Society) waliokuwa wakifanya kazi huko Nyanda za Juu Kusini nchini Tanzania walikutana na wawindaji ambao waliwaeleza kuwa kulikuwa na nyani anayeitwa kipunji katika misitu ya Mlima Rungwe. Walishangaa kwa kuwa hawakuwahi kuwaona nyani hao lakini wenyeji wa huko ambao ni Wanyakyusa ni wasimulizi wazuri wa hadithi, ingawa wakati mwingine ni vigumu kujua ukweli wa simulizi za asili za wenyeji.
Mwezi Mei mwaka huo huo, wakati watafiti hao wakishughulika na mambo ya bioanuai maeneo ya Nyanda za Juu Kusini, waliwaona kwa mara ya kwanza nyani ambao si wa kawaida. Ilichukua miezi mingi kuwafuatilia nyani hao ambao mara nyingi hupenda kujificha kabla ya kuwaona vizuri na kupata picha. Hapo ndipo walithibitisha bila shaka yoyote kuwepo kwa nyani aina ya kipunji mwenye rangi ya kahawia, uso mweusi, mdomo kama wa kima na sauti ya juu. Hii ilikuwa aina mpya ya nyani kwa wanasayansi wa nchi za magharibi.
Kwa bahati ya pekee, mwezi Julai 2004 watafiti waliokuwa wakifanya kazi eneo la Milima ya Udzungwa takriban kilometa 350 (maili 220) upande wa kaskazini mashariki, waliwaona aina ya nyani ambao waliamini hawajawahi kuonekana na watafiti wengine. Mwaka uliofuata, yaani 2005, makundi hayo mawili ya watafiti kwa pamoja yalichapisha taarifa ya utafiti wao katika jarida la Science wakielezea aina hiyo mpya ya nyani. Mwanzoni waliwaita mangabey wa milimani (Lophocepus kipunji), lakini baada ya uchambuzi wa vinasaba vya mnyama aliyekufa wakawapa jina la kipunji (Rungwecebus kipunji), ambalo ni utambulisho wa kipekee kwa kuwa hawakufanana na nyani mwingine wa aina yoyote. Utafiti huo ulifanya kipunji kuwa aina mpya ya nyani iliyopatikana kwa zaidi ya miaka 80.

Lakini msisimko wa kugundua aina mpya ya nyani ulileta wasiwasi. Kipunji, makazi yake ya misitu na bioanuai husika ambavyo havipatikani kwingineko ulimwenguni vilikuwa hatarini. Mlima Rungwe na Safu ya Milima ya Livingstone iliyopo Nyanda za Juu Kusini ndiko wanakoishi asilima 95 ya kipunji. Eneo hili siyo hifadhi ya taifa kwa hiyo ukataji miti, uchomaji mkaa na ujangili vilikuwa vimeshamiri.
Wakulima walikuwa wamepanua mashamba yao mpaka ukingoni kabisa mwa msitu, ikiashiria hatari ya kuigawa ikolojia na kutenganisha makundi mawili ya kipunji.
Katika Milima ya Udzungwa ambako watafiti walikuwa wamegundua kundi la pili la kipunji msitu ulikuwa haujaathirika sana lakini hapa palikuwa na kipunji wachache.
Kulingana na sensa ya kwanza iliyofanyika 2007, kulikuwa na jumla ya kipunji 1,117 katika milima yote.
“Tulipata msisimko mkubwa kutokana na kugundua aina hii ya nyani, lakini pia ulikuwa ugunduzi muhimu,” anasema Mkurugenzi Mstaafu wa Uhifandhi wa Aina Muhimu za Wanyama na Sayansi wa Shirika la WCS kwa upande wa Afrika, Tim Davenport. Ugunduzi huo uliamsha mshawasha wa jumuiya za kimataifa, msaada kutoka kwa wanasiasa na hivyo kuleta fedha kwa ajili ya utafiti na kuwawezesha WCS kufanya kazi na serikali na jamii katika uhifadhi jumuishi wenye malengo ya muda mrefu.
Programu ya uhifadhi ilifanikiwa kwa kuwa sensa ya hivi karibuni imeonyesha kuwa kwa miaka 13 iliyopita, idadi ya kipunji katika milima ya Nyanda za Juu Kusini imeongezeka kwa asilimia 65, na wamesambaa kwa takriban moja ya tano ya eneo. Wakati huo huo, shuguli za binadamu katika maeneo hayo zimepungua kwa asilimia 81. Takwimu hizi ni kulinagana na ripoti ya mwaka 2022 iliyochapishwa na International Journal of Primatology paper.


Davenport anasema kuwa wakati alipoanza kufanya kazi mwaka 1999, kulikuwa na taarifa chache sana kuhusu bioanuai ya milima ya Nyanda za Juu Kusini. Eneo hilo halina wanyama wakubwa kama ilivyo katika hifadhi za taifa za kaskazini kama Serengeti. Wala maeneo yenye bioanuai ya kipekee kama ya Milima ya Udzungwa hayakuwa maarufu. Lakini maeneo hayo yalikuwa na mbuga za milimani za kushangaza, udongo wa volcano wenye rutuba, na mvua za kutosha, lakini vyote vilikuwa havijagunduliwa. Katika mazingira hayo haikuwa rahisi kuwagundua nyani ambao ni adimu. Sophie Machaga alianza kufanya kazi na WCS na sasa ni Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Nyanda za Juu Kusini wa shirika hilo. Anakumbuka siku zile ambapo timu ya watafiti ilitembea kwa miguu umbali mrefu kwenye makorongo yenye kina kirefu na misitu minene ikiwatafuta kipunji.
“Ilikuwa kama mchezo…unawaona halafu ghafla wanapotea….halafu unawaona tena. Wakati mwingine ulikuwa unaweza kuwaona na ukawafuatilia kwa masaa kadhaa halafu ghafla wakahamia kwenye eneo jingine ambako huwezi kuwafuata kwa sababu ya makorongo. Kwa hiyo huwaoni tena!” anasema Machaga.
Na nyani hawa huishi kwenye misitu ya milimani yenye urefu wa kati ya mita 1,300 na 2,450 (futi 4,270-8,040) kutoka usawa wa bahari katika makundi ya wanyama kuanzia 15 mpaka 30. Huishi kati ya dari zilizojengwa kwa miti wakila aina mbalimbali ya majani, magome ya miti, matunda, mbegu na wadudu.

Utafiti pia uliangalia migongano ya wanyamapori na binadamu. Wakulima wa maeneo ya Mlima Rungwe na Mlima Livingstone hulima ndizi, mahindi, viazi na wakati mwingine aina mbalimbali za mboga kama karoti. Pamoja na aina walizonazo, nyani hawa wakati mwingine huvinjari ukingoni mwa misitu ili kuvamia mashamba ya mazao, tabia ambayo inawafanya wakulima kuweka mitego hatari ili kuwanasa.
Machaga anaeleza alivyoshuhudia nyani hao wakivamia shamba wakati akifanya uchunguzi katika maeneo ya Rungwe ili kubaini kiwango cha uharibifu ambao nyani wanafanya. Palikuwa na shamba pembezoni mwa msitu na katikati ya shamba kulikuwa na kibanda ambamo mkulima alitundika mahindi ili yakauke. Mkulima alipoondoka, nyani mmoja akapanda juu ya mti akaangalia huku na huko na baada ya kuona hapakuwa na mtu yeyote aliwaita wenzake.
![]() Vijiji katika Nyanda za Kusini hutegemea kuni kwa kupikia. Kwa ujumla shughuli za binadamu katika maeneo wanayokaa kipunji zimepungua kwa asilimia 81 katika kipindi cha miaka 13 kutokana na uhifadhi jumuishi. Ukataji miti kwa kutumia misumeno ya asili na kuchoma mkaa vimepotea katika eneo la Mlima Rungwe na Mlima Livingstone ambako kipunji wanapatikana. Picha na Tim Davenport. |
“Sasa fikiria takriban nyani 30 wanavamia shamba, wengine wakaingia kwenye kibanda na kuchukua mahindi wakakimbia na kuwapa wenzao kisha wakarudi tena kuchukua mengine. Nilimwonea huruma yule mkulima; labda itabidi tumpe fidia fulani japo siyo sisi tulioiba mahindi yake,” anaeleza Machaga.
Ili kupunguza migongano, watafiti kutoka WCS walijaribu njia kadhaa ikiwemo kupaka mafuta yenye pilipili na kinyesi cha ngombe kwenye mabua ya mahindi wanapoingilia nyani kutoka msituni. Wakulima pia walibadili mpangilio wa mazao katika mashamba yao wakipanda parachichi na viazi pembezoni mwa mashamba ambavyo nyani hawavipendi.
Tishio jingine walilokabiliana nalo kipunji ni uharibifu wa makazi yao unaosababishwa na ukataji miti kwa ajili ya mbao na kuchoma mkaa na mitego ya asili inayotegwa na wawindaji ndani ya msitu.
“Haihitaji utaalamu wa hali ya juu kumaliza matatizo haya. Ni kufahamu mahitaji ya watu na kujaribu kuyatekeleza,” anasema Machaga. “Tunahitaji kufanya kazi na serikali ili kuboresha usimamizi wa sheria za misitu na uhifadhi katika eneo hili la Nyanda za Juu Kusini”.
Eneo la Milima ya Livingstone limeingizwa katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo. Mlima Rungwe umepandishwa hadhi na kuwa hifadhi ya asili na WCS imekodi eneo la tatu la mlima unaokaliwa na kipunji linaloitwa Nkuku kwa nia ya kuwa hifadhi binafsi ambako kipunji wanaweza kuishi na kufanyiwa utafiti na baadaye kuwa eneo la uhifadhi.
Kadhalika, WCS ilitoa msaada wa fedha na wa kiufundi katika kusimamia maeneo hayo. Misaada hiyo ni pamoja na kuajiri askari wa wanyamapori na kuwapa mafunzo na kuweka mipaka ili watu wafahamu wanapoingia eneo la msitu, na kuondoa mitego mara kwa mara.
Vivutio kwa jamii za wenyeji ni kuwepo kwa fursa za kiuchumi, kutoa mbadala wa kukata miti katika makazi ya kipunji, kwa ajili ya mbao, mkaa na ujangili. Kufanya kazi kwa karibu na watendaji wa serikali kama huduma za misitu kuliwasaidia WCS kuanzisha misitu midogo kwa ajili ya kuni, kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki kwa ajili ya asali ili jamii ijiongezee kipato, kuanzisha kikosi cha askari jamii wa wanyamapori na kuwasaida wenyeji kuanzisha vitalu vya miti ya asili kwa ajili ya kurejesha uoto wa asili.
WCS kwa kushirikiana na serikali pia ilianzisha mpango wa kutoa elimu kwa vijiji vilivyopo ndani ya kilomita tano (maili tatu) kutoka kwenye hifadhi.
Mafunzo hayo ni pamoja na kuanzisha vilabu vya wanyamapori katika shule za msingi na sekondari, kuandaa sinema na programu maalumu za elimu ya watu wazima zilizolenga umuhimu wa misitu kwa ajili ya upatikanaji wa maji na faida nyingine za ikolojia.

Pamoja na kwamba baadhi ya shughuli za WCS zimefikia tamati, watu bado wameacha ukataji miti na uwindaji. Na wakiona baadhi yao wanaendesha shughuli hizo, hutoa taarifa kwa WCS au mamlaka husika. “Hii inaonyesha kuwa jamii inathamini misitu na kuona kuwa wanaimiliki wenyewe,” alisema Machaga.
Ni wazi kwamba njia za uhifadhi ambazo watafiti wamezitumia katika miaka 20 iliyopita zimefanikiwa kwani idadi ya kipunji imeongezeka na wanyama hao sasa hawamo tena kwenye orodha ya wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka.
Hata hivyo, idadi ya kipunji, ambayo sasa imefikia 1,966, na ikijumuishwa na idadi ya udzungwa, kwa kiwango cha kuhofisha, na imeainishwa kwenye Orodha Nyekundu ya IUCN kama spishi iliyo hatarini kuangamia.
Profesa Mshiriki wa ikolojia katika Chuo Kiuu cha Florence, Italia, na mtafiti katika kituo cha Ecological Monitoring Centre cha Udzungwa, Tanzania, Francesco Rovero, anasema idadi ndogo ya kipunji katika milima ya Udzungwa yenye wanyama kati ya 60 na 150, imebaki hivyo kwa muda mrefu kulingana na uchunguzi uliofanywa kati ya mwaka 2006 na 2016.
Misitu iliyoko katika Milima ya Udzungwa haifikiki kwa urahisi na hali yake ni nzuri lakini inashangaza kwanini idadi ya nyani hao haiongezeki. “Huenda hao ni masalia ya kundi kubwa zaidi lililokuwepo huko na halikuweza kuzaliana au linakabiliwa na mapambano na aina nyingine ya nyani kama Sykes (Cercopithecus albogularis). Inawezekana pia makazi yao siyo rafiki. Hakuna jibu la mkato,” anasema Rovero.

Sasa, hatma ya kipunji iko mikononi mwa serikali na jamii za wenyeji katika maeneo ya misitu husika. Davenport anasema kuwa asasi za kimataifa ni kiunganishi tu kati ya makundi hayo mawili na siyo jukumu lao kuwepo kila wakati.
“Siku zote tunafikiria kufika mwisho wa shughuli zetu. Na sasa kuna fursa nyingi za uhifadhu. Wapo wanaoshughulika na utalii, wapo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na Mamlaka ya Hifadhi ya Mbuga za Taifa, na wote wanafanya kazi nzuri. Mambo hayajakamilika; bado kuna shinikizo mbalimbali, kuna uvunjifu wa sheria kama ilivyo katika nchi nyingi hapa duniani, na bado kuna umaskini. Lakini mambo yamekuwa mazuri zaidi kuliko hapo zamani,” Anasema Davenpot.
Picha ya bango: Kipunji huishi kwenye misitu iliyoko milimani yenye urefu wa mita 1,152 hadi 2,450 kutoka usawa wa bahari kutokana na sensa iliyofanyika hivi karibuni. Hulala kwenye makorongo marefu na pembezoni mwa mabonde. Picha na Tim Davenport.
Nukuu:
Jones, T., Ehardt, C. L., Butynski, T. M., Davenport, T. R., Mpunga, N. E., Machaga, S. J., & De Luca, D. W. (2005). The highland mangabey Lophocebus kipunji: A new species of African monkey. Science, 308(5725), 1161-1164. doi:10.1126/science.1109191
Davenport, T. R., Stanley, W. T., Sargis, E. J., De Luca, D. W., Mpunga, N. E., Machaga, S. J., & Olson, L. E. (2006). A new genus of African monkey, Rungwecebus: Morphology, ecology, and molecular phylogenetics. Science, 312(5778), 1378-1381. doi:10.1126/science.1125631
Davenport, T. R., De Luca, D. W., Jones, T., Mpunga, N. E., Machaga, S. J., Kitegile, A., & Phillipps, G. P. (2008). The critically endangered kipunji Rungwecebus kipunji of southern Tanzania: First census and conservation status assessment. Oryx, 42(3), 352-359. doi:10.1017/S0030605308000422
Davenport, T. R., Machaga, S. J., Mpunga, N. E., Kimiti, S. P., Mwalwengele, W., Mwaipungu, O., & Makumbule, P. M. (2022). A reassessment of the population size, demography, and status of Tanzania’s endemic Kipunji Rungwecebus kipunji 13 years on: Demonstrating conservation success. International Journal of Primatology, 43(2), 317-338. doi:10.1007/s10764-022-00281-3
Barelli, C., Oberosler, V., Cavada, N., Mtui, A. S., Shinyambala, S., & Rovero, F. (2023). Long‐term dynamics of wild primate populations across forests with contrasting protection in Tanzania. Biotropica, 55(3), 617-627. doi:10.1111/btp.13212
Mittermeier, R. A., Ratsimbazafy, J., Rylands, A. B., Williamson, L., Oates, J. F., Mbora, D., … Aguiar, J. M. (2007). Primates in peril: The world’s 25 most endangered primates, 2006–2008. Primate Conservation, 22(1), 1-40. doi:10.1896/052.022.0101
Mittermeier, R. A., Wallis, J., Rylands, A. B., Ganzhorn, J. U., Oates, J. F., Williamson, E. A., … & Schwitzer, C. (2009). Primates in peril: the world’s 25 most endangered primates 2008–2010. Primate Conservation, 24(1), 1-57. doi:10.1896/052.024.0101
Schwitzer, C., Mittermeier, R.A., Rylands, A.B., Chiozza, F., Williamson, E.A., Byler, D., Wich, S., Humle, T., Johnson, C., Mynott, H., and McCabe, G. (eds.). 2019. Primates in Peril: The World’s 25 Most Endangered Primates 2018–2020. IUCN SSC Primate Specialist Group, International Primatological Society, Global Wildlife Conservation, and Bristol Zoological Society, Washington, D.C.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 05/07/2023.
